WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki ameagiza maafisa mifugo na madaktari wa mifugo, Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, walioandika au kushuhudia vyeti vya vifo vya ng’ombe zaidi ya 270 ambao walikamatwa na uongozi wa Pori la Hifadhi la Maswa kusakwa na kufikishwa katika Baraza la Veterinari Tanzania ili kuchunguzwa.
Waziri Ndaki amebainisha hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya za Itilima na Meatu ambapo akiwa katika Wilaya ya Itilima aliarifiwa baadhi ya wafugaji walioshinda kesi Mahakama ya Rufaa mwaka 2019, baada ya ng’ombe wao kudaiwa kuingia katika Pori la Hifadhi la Maswa mwaka 2017, kurejeshewa ng’ombe 51 pekee huku uongozi wa pori hilo ukiwaarifu ng’ombe zaidi ya 270 walikufa, bila wafugaji hao kushuhudia mizoga ya ng’ombe hao wala vyeti vya vifo ambavyo inaelezwa viliandikwa na maafisa mifugo ambao pia hawakushudia mizoga hiyo.
Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa sasa inafuatilia taarifa za wafugaji kote nchini, ambao mifugo yao ilikamatwa na baadaye wafugaji hao kushinda kesi lakini mifugo hiyo haijareshwa kwao wala fedha walizolipishwa faini, kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutaka taarifa hiyo ambayo wizara inakusanya ili kuifikisha kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa ajili ya maamuzi zaidi.
“Maafisa mifugo na madaktari wa mifugo nchi nzima mnapaswa kujua nyie ni madaktari wa mifugo siyo kukaa kwenye meza na kuandika vyeti vya vifo vya ng’ombe bila kushuhudia vifo hivyo, baadhi yenu wanafanya kazi kiholela.” Amesema Mhe. Ndaki
“Hili jambo siyo dogo ni kubwa nimeagizwa na Rais nije kufuatilia masuala haya watu wameshinda kesi lakini ng’ombe hawajarudishwa kwa wenyewe, nimeambiwa nifuatilie nipeleke orodha yote kwa waziri mkuu ili taarifa itolewe.” Amefafanua Ndaki.
Kuhusiana na ng’ombe zaidi ya 270 ambao hawajulikani walipo Waziri Ndaki amemjulisha afisa mifugo Mkoa wa Simiyu kwamba wizara inataka kujua aliyeandika vyeti vya vifo vya ng’ombe hao ambavyo havijulikani vilipo na wala ushahidi wa kuwa ng’ombe hao walikufa, huku akionya maafisa mifugo na madaktari watakaobainika kuendelea kufanya kazi bila kufuata taratibu za kazi zao Baraza la Veterinari Tanzania halitasita kufuta usajili wao.