MREMBO Wema Isaac Sepetu anadaiwa kumvuruga kabisa mzazi mwenza wa staa wa muziki nchini Tanzania, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, IJUMAA WIKIENDA lina mambo mazito.
Itakumbukwa kwamba, Wema na Diamond au Mondi ni wapenzi zilipendwa ambao kapo yao ilitia fora ndani na nje ya Bongo kipindi kile cha Wimbo wa Nimpende Nani.
CHANZO CHA YOTE
Chanzo cha vurugu yote ni baada ya hivi karibuni Mondi kuposti video yake mpya ya Wimbo wa Nitaanzaje na kuandika; “Nikiitazama hii video, hususan kipande hiki, nakumbuka mbali sana… enzi za mahaba mazito na Madam (Wema Sepetu)…. Enzi ambazo tulikuwa tunajifungia chumbani wiki nzima, nakwepa ku-record na hata show ikitokea naitafutia sababu ya kutokuwepo….
“Kiukweli wimbo huu wakati nautoa, sikuuchukulia serious….niliutoa tu kama bonasi kwa kujua mashabiki wangu wamenimiss kunisikia nikiimba hivyo…
“Licha ya kupokelewa na kupendwa sana ulivyotoka… for some reason kadiri muda uendavyo nimejikuta naupenda saana na mbaya zaidi kila niusikiapo unanifanya nitamani tena kumpenda mtu na kuwa tena wenye mahusiano…… japo ghafla akili timamu hunijiaga na kuniambia ‘Simba ji-focusie zako kwenye kazi mwaya…”
Kwa sasa, maneno hayo yamesababisha vita kati ya Mondi na Zari ni ya waziwazi kwani kinachoendelea kati yao ni mwendo wa kurushana roho tu.
ZARI AJIBU MAPIGO NA MR P
Mara tu baada ya Mondi kumsifia Wema wikiendi iliyopita kuwa amelimisi penzi lake, Zari naye alijibu mapigo kwa kumposti aliyekuwa memba wa Kundi la P-Square, Peter Okoye ‘Mr P’ kwenye Insta Story yake na kumuweke maneno matamumatamu akionesha kumsapoti katika kazi zake.
Jambo hilo linasemekana kumtibua kabisa Mondi ambaye naye ameendelea kujibu mashambulizi kwani inasemekana ni kama ametoneshwa kidonda kwa sababu alishamtuhumu jamaa huyo kutoka na Zari enzi zile wakiwa ni wapenzi.
Katika moja ya intavyu zake, Mondi aliwahi kukiri kwamba, wakati akiwa na Zari moja ya mambo yaliyomtesa ni pamoja na kujua kwamba, mwanamama huyo alichepuka na Mr P.
FAMILIA YA MONDI YAUNGA MKONO
Katika hali kama hiyo, familia ya Mondi ikiongozwa na mama yake mzazi, Sanura Kassim au Mama Dangote, Esma Platnumz na Rommy Jones wamemuunga mkono staa huyo wa Ngoma ya Nitaanzaje kwa kuendelea kumpaisha Wema na kumpamba ile mbaya.
Hata hivyo, vyanzo vya ndani ya familia ya Mondi vimekiri na kueleza sababu ya uwepo wa vita hiyo nzito.
Chanzo cha habari kinadai kuwa, mwishoni mwa mwaka jana na mapema mwaka huu, Mondi na Zari walimaliza tofauti zao zilizosababisha waachane siku ile ya Valentine ya Februari 14, 2018 na hata kukubaliana kufanya kipindi chao cha maisha halisi (reality show) kinachokwenda kwa jina la Young, Famous and African (Mwenye Umri Mdogo, Mashuhuri na Mwafrika) ambacho kinatarajiwa kuanza hivi karibuni kupitia Kampuni ya Netflix.
ZARI AHISI KUTUMIKA, HARMONIZE ATAJWA
Kuna madai mazito yanasemwa kwamba, kuna wakati Zari alihisi kama Mondi anataka kumtumia vibaya katika kiki zake za kumzima msanii Harmonize Konde Boy Mjeshi ambaye aliona kama anataka kumzidi nguvu hivyo akaweka mgomo wa hata kumleta Bongo mtoto wao, Tiffah Dangote kwa ajili ya pati kubwa ya birthday ambayo jamaa huyo alitaka kuiandaa.
Maelezo ya Team Zari ni kwamba, mwanamama huyo hakutaka kutumika kwenye jambo ambalo alidai kwamba, haoni faida atakayoipata na hapo ndipo akawa amemtibua Mondi na mambo yakaanza kwenda mrama na kilichofuata ni kurushana roho kama kote.
TATIZO LINGINE
Baada ya kutofautiana kwa wawili hao ndipo Mondi anatajwa kuibua tatizo lingine baada ya kufuta picha na video zote za wanawe, Tiffah Dangote na Prince Nillan aliozaa na Zari, jambo ambalo limezidi kumtibua mwanamama huyo kwa sababu yupo radhi afanyie mambo mabaya yeye na siyo watoto.
“Sijali watu watasema nini juu yangu, cha msingi ni furaha ya watoto wangu,” alisema Zari alipotua Bongo kuwaleta wnawe hao kwa baba yao, Mondi au Simba wa Tandale.
NI KIKI?
Baadhi ya watu wanakwenda mbali zaidi na kudai kwamba, yote hayo yanayoendelea, lengo kuu ni kutafuta kiki kwa ajili ya wimbo huo mpya wa Mondi wa Nitaanzaje.
Baadhi ya watu wa karibu wa Wema wamechukizwa na kitendo cha familia hiyo kutaka kumtumia kwa ajili ya kiki zao na kumtaka mrembo huyo kutotoa kiki hiyo, lakini mwanadada huyo amewashangaza baada ya kuibuka na ishu ya kumisi vipigo vya jamaa huyo.
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta Wema kujua anachukuliaje ishu hiyo ambapo pamoja na kupewa maelezo marefu juu ya kile kinachoendelea, mwenyewe amejibu kwa kifupi; “No comment…” akimaanisha hana la kusema.