BAADA ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Rivers United ya Nigeria kwenye mchezo wa kwanza hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa wikiendi iliyopita katika Dimba la Mkapa, Dar, mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba amefunguka kuwa timu hiyo ina nafasi ya kupindua meza mchezo wa marudiano.
Yanga ina kibarua kigumu dhidi ya Rivers United kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa Septemba 19, mwaka huu nchini Nigeria ambapo kikosi hicho kinachonolewa na Naserddine Nabi, kinahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili waweze kufuzu hatua inayofuata ya michuano hiyo.
Akizungumza na Spoti Xtra Mziba alifunguka kwamba: “Yanga bado wana nafasi ya kupindua matokeo kwenye mchezo wa marudiano, kama Rivers wameweza kupata matokeo hapa, basi Yanga nao wanaweza kupata matokeo mazuri Nigeria. Kikubwa benchi la ufundi wajikite kuyafanyia marekebisho mapungufu yaliyojitokeza ili yasijirudie.
“Mashabiki hawapaswi kukata tamaa bali wawaamini wachezaji wao na lolote linaweza kutokea kwenye mchezo wa marudio na Yanga wanaweza kupata matokeo mazuri na kusonga mbele.”