MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli, amesema sababu ya kualika watu wengi kusafiri na timu Nigeria ni kuongeza hamasa kwa wachezaji ndani na nje ya uwanja.
Bumbuli alisema wanajua ugumu wa mchezo wa marejeano wakiwa ugenini dhidi ya Rivers United, hivyo vita hiyo hawawezi wakaishinda bila msaada wa watu wengine nje ya uwanja.
Yanga waliondoka jana Ijumaa kwenda nchini Nigeria wakiwa na msafara wa jumla ya watu 100, ambapo watakuwa na wachezaji 23, watu sita wa benchi la ufundi na idadi itakayobaw kia ni ya watu ambao wamealikwa.
“Msafara wetu una watu takribani 100, kwa maana ya wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na Wanayanga wengine ambao tumewapa mualiko wa kuongozana na sisi.
“Hii mechi ni zaidi ya mechi ambayo tunahitaji kupata matokeo mazuri ili tuweze kusonga mbele, kwa hiyo watu tunaoondoka nao tunaamini wanakwenda kuwa chachu kwa asilimia fulani kwa wachezaji,” alisema Bumbuli.
Issa Liponda, Dar es Salaam