Babati. Mkazi wa Kijiji cha Riroda, wilayani Babati mkoani Manyara, Monica Manyara (65), amefariki dunia baada ya kujinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya katani.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Manyanya kabla ya kifo chake hiki, alishawahi kujaribu kujinyonga zaidi ya mara tatu kwa siku tofauti lakini alinusurika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Merrisone Mwakyoma aliliambia Mwananchi jana ofisini kwake, kwamba Manyanya alijinyonga Oktoba 13.
Kamanda Mwakyoma alisema chanzo cha Manyanya kujinyonga hakijajulikana mara moja ila polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Alisema kabla ya kifo chake, Manyanya alitoweka nyumbani kwake tangu Oktoba 8 mwaka huu.
“Ndugu zake walimtafuta kwa siku zote hizo hadi wakamkuta kajinyonga mlimani kwa kamba siku hiyo ya tukio,” alisema kamanda Mwakyoma.
Alidai kuwa marehemu huyo alikuwa na tatizo la afya ya akili kwa sababu alishajaribu kujinyonga zaidi ya mara tatu lakini alinusurika kufariki dunia.
“Ndugu zake ndiyo waligundua kutokea kwa kifo hicho na wao ndiyo wakatoa taarifa kwa Mwenyekiti wa kijiji ambaye aliwasiliana na polisi waliofika eneo la tukio,” alisema kamanda Mwakyoma.
Alisema Polisi waliufanyia uchunguzi mwili huo na kuukabidhi kwa ndugu zake kwa ajili ya maziko.
“Natoa wito kwa wananchi wakimuona mtu anajaribu kujinyonga kutoa taarifa kwenye ofisi za ustawi wa jamii au polisi ili apatiwe ushauri wa kisaikolojia,” alisema kamanda Mwakyoma.
Jirani wa marehemu, Rose Elvis alisema wamesikitishwa na tukio hilo kwani Manyanya alishajaribu kujiua zaidi ya mara tatu ila hakufanikiwa.