“Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa Julius Kambarage) angekuwepo na kushuhudia yanayotokea nchini kwa sasa angepasuka moyo, angepiga watu viboko hadharani na pengine angemwomba Mungu aichukue roho yake kama alivyofanya Nabii Musa nikitumia mfano wa maandiko ya Biblia Takatifu.”
Hiyo ni kauli ya Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi akizungumzia miaka 22 ya kifo cha Hayati Julius Kambarage Nyerere.
Kiongozi huyo wa kiroho anasema Mwalimu Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza alikokuwa anatibiwa, angekuwa hai hadi leo, angewaadhibu hadharani baadhi ya viongozi kuanzia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi serikalini kutokana na mmomonyoko wa maadili.
“Uadilifu wa baadhi ya viongozi waliokabidhiwa dhamana ya ofisi za umma unatiliwa mashaka sana ndiyo maana matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma umekuwa jambo la kawaida. Tumemsikia Rais Samia Suluhu Hassan akitishia kuonyesha rangi zake halisi iwapo fedha za kukabiliana na athari za Uviko-19 zitatumika vibaya,” anasema.
Huku akichukua tahadhari kwa kuchagua maneno na hoja zake, Askofu Niwemugizi anataja baadhi ya maeneo anayoamini yangemsononesha Mwalimu Nyerere iwapo angekuwa hai hadi leo kuwa ni kummonyoka kwa maadili ya uongozi, kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali na fedha za umma, ubinafsi na matumizi mabaya ya madaraka na ofisi.
“Siyo kwamba hakukuwa na tuhuma au vitendo vya rushwa wakati wa Mwalimu Nyerere. Vilikuwepo. Lakini viongozi wa wakati ule waliposema wanachukia rushwa ilionekana kweli wanaichukia kwa maneno na matendo vyao tofauti na sasa ambapo kuchukia rushwa imekuwa suala la maneno bila vitendo,” anasema.
Kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja, anasema Mwalimu Nyerere angefanya kila njia kusahihisha mambo ndani ya CCM ambacho ndicho kinaongoza dola na iwapo ingeshindikana, angetoka hadharani kukosoa na kutoa mwongozo, pengine kujitoa CCM.
“Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa uhuru wa mawazo, mijadala na kujenga hoja. Alipenda kuona jamii ya watu wanajadiliana kwa hoja hata pale wanapokinzani kimtazamo. Hakupenda hoja za upande mmoja ndiyo maana licha ya wenzake ndani ya CCM kupinga mfumo wa vyama vingi, yeye alishauri uruhusiwe,” anasema Askofu Niwemugizi.
Anasema hali imebadilika siku hizi ambapo hoja hazijibiwi kwa hoja imara na bora zaidi, bali nguvu na mamlaka ya dola.
“Hoja za upande wa upinzani zikionekana kuwa na nguvu, basi nguvu ya dola hutumika kuzizima huku mwenye maoni tofauti na utawala akionekana kuwa siyo mzalendo. Mwalimu Nyerere alikuwa tayari kusikiliza maoni ya wengine hata kama hakubaliani nayo na kuyajibu kwa hoja,” anasema.
Anasema siyo ajabu hivi sasa kuona vyombo vya dola vikitumika kuzima fikra, mawazo na sauti za watu wenye mawazo kinzani na yale ya mfumo wa uongozi na kuna hisia inaanza kujengeka ndani ya jamii kuwa kuna upendeleowa haki za kisiasa na kiraia ambapo walioko nje ya mfumo wa utawala wanazuiwa kusema au kufanya ambayo walioko ndani wanafanya.