Askofu Shoo: Mungu amemleta Samia kuponya majeraha


Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amewataka viongozi wenye mamlaka kusimama kwenye nafasi zao kwa uaminifu ili kuponya majereha ya watu.
Pia, amekumbushia jinsi hotuba ya kwanza aliyoitoa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiapishwa ilivyogusa majeraha ya maisha ya Watanzania na kuwaponya majeraha na kwamba, Mungu amemleta duniani kwa makusudi yake ili aponye majeraha hayo.

Askofu Shoo ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 16, 2021 wakati wa ibada ya shukrani ya Maadhimisho ya miaka 50 ya Jubilei ya Hospitali Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC).

Amesema ni wajibu wa wote ambao Mungu amewapa mamlaka na nafasi ya kuwa viongozi kutimiza wajibu kwa unyenyekevu, uaminifu na upendo.

Pia, amesema ni wajibu wa watawala kutawala kwa kadri ya mapenzi ya Mungu, na kuonyesha kuwa hakuna anayeonewa wala kulia kwa sababu ya kukosa haki za msingi.

Pia, amewataka viongozi wa dini kutimiza wajibu kuhakikisha watu wanapata afya ya kiroho na kiakili kwa kuwakumbusha kuishi maisha ya kumcha Mungu na kujutia dhambi zao.

"Viongozi na watawala simameni katika nafasi zenu kwa uaminifu ili ahadi ya Mungu ya kurudishia taifa letu afya, kutupa ustawi wa kweli na kutuponya jeraha lipate kutimia.

"Rais na viongozi wengine tujue tumewekwa kwa kusudi la Mungu, tuombe tutimize mapenzi ya Mungu na tutambue tuna wajibu wa kutenda haki ili miaka 50 ijayo tuwe na cha kukumbukwa.

"Hakika Rais wetu tumesikia kuheshimiwa, Mungu amekuweka kwa kusudi, mama Mungu akuwezeshe," amesema Askofu Shoo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad