Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imebaini kuwa mashine mpya za kutengeneza vitambulisho vya Taifa, zimeshindwa kufanya kazi kutokana na kukosa karatasi zinazoweza kutumiwa na mashine hizo.
Hali hiyo imefanya Mamlaka ya Vitambulisho Nchini (Nida) kutengeneza vitambulisho 250 badala ya vitambulisho 4,500 kwa saa ambayo ni ahadi waliyoitoa bungeni mara baada ya kununua mashine mpya za kutengeneza vitambulisho.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka baada ya kuchambua ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka huu.Alisema kamati hiyo haikuridhishwa na jinsi Nida ilivyojibu hoja za kikaguzi za CAG na kwamba hata walipofika katika kamati hiyo, walishindwa kuelezea kwa ufasaha katika maeneo mengi.
“Imeonekana Nida hawakutimiza maagizo waliyopewa na kamati hii katika mwaka 2019/2020. Tumewapa Nida maagizo kuwa katika wiki mbili kuanzia leo (jana) wawasilishe kwa CAG na nakala walete kwa Katibu wa Bunge majibu sahihi ya hoja zote zilizotokewa na CAG,”alisema.
Kaboyoka alisema hadi jana Nida walikuwa hawajatendea haki maagizo waliyopewa na kamati yake.
Alisema agizo jingine ni kutengeneza vitambulisho ambapo katika Bunge lilopita wabunge walielezwa kuna mashine mpya zimenunuliwa ambazo zitatengeneza vitambulisho vingi.
“Lakini matokeo yake kumetokea utata mkubwa ambapo hata mashine zilizoletwa, hakuna karatasi zilizoletwa kwa ajili ya kutengenezea vitambulisho hivyo ambavyo vingetengenezwa kwa wingi,”alisema.
Kaboyoka alisema matokeo yake wamerudi nyuma kwa kutumia karatasi za zamani ambazo walisema kuwa zisingeweza kutumiwa na mashine hizo mpya.
Alisema kwa mashine mpya hizo zingetengeza kadi 4,500 kwa saa, lakini sasa wanatengeneza 250 kwa saa na hivyo itachukua muda mrefu Watanzania kupata vitambulisho vya Taifa.
Aliyataja maagizo mengine waliyoyatoa kwa Nida ni pamoja na kuweka utambulisho wa mali za mamlaka hiyo na kupata hati za viwanja vyote.
Hata hivyo, alisema hadi jana kati ya viwanja 152 ni 11 tu ndio vilivyopata hati miliki.
Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Japhat Hasunga, alisema Nida tangu waanze kufanya kazi hiyo walikuwa wametoa vitambulisho milioni sita na mwaka huu utakapoisha wanatarajia kutengeneza vitambulisho milioni 4.5 na hivyo kufanya vitambulisho milioni 10.5.
“Sasa ukilinganisha na mahitaji ya Watanzania ambao ni karibu watu milioni 30 wanaohitaji vitambulisho, kamati inaona hili jukumu litaisha lini, kama hatua yenyewe ni hii?
‘‘Na kama mashine hizo hadi sasa wanasema hawana malighafi hili jukumu walilopewa na Watanzania, hivi vitambulisho vitapatikana lini?”alihoji.
Alisema mamlaka hiyo ya vitambulisho, ilinunua mashine za awali tatu za kutengenezea vitambulisho, lakini hazikuwezesha kufikia malengo ya kutengeneza vitambulisho.
“Kwa hiyo yale matumizi ambayo walitumia kununua mashine yamepotea, sasa wamenunua mashine tena mpya hawana malighafi za kutengeneza vitambulisho kisasa, hivyo unakuta karibu mwaka mzima wanacheza bado wanasema wana matatizo ya kimkataba,”alisema.