KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka, ameagiza kukomeshwa mara moja vitendo vya unyanyasaji wa wananchi katika Jimbo la Ushetu, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Miongoni mwa manyanyaso hayo ni ukamataji wananchi usio na staha hususan kwa wale wanaodaiwa kukutwa na mazao ya misitu ikiwamo mkaa.
Pia amelitaka Jeshi la Polisi wilayani Kahama kuwatazama baadhi ya askari wake wanaodaiwa kuwabambika kesi wananchi kwa madai ya kukamatwa na bangi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Ushetu uliofanyika Kijiji cha Iboja juzi, Shaka alisema CCM hataki kusikia aina yoyote ya unyanyasaji dhidi ya wananchi.
"Nimeelezwa na wananchi kuwa moja ya changamoto hapa Ushetu ni maofisa wa TFS (Wakala wa Huduma za Misitu) kuwakamata katika namna ya manyanyaso ikiwamo kuwadhuru na kuwaharibia vifaa vyao kama baiskeli wanazozitumia kusafirisha mkaa.
"Jambo hili sio sawa, kama kuna tatizo, njia bora ya kukabiliana nalo ni kutumia namna sahihi za kisheria, siyo kuwashambulia, kuwaharibia vifaa na wakati mwingine kuwadhuru maungoni," alisema.
Shaka alisema wapo baadhi ya askari polisi wanatumia kisingizio za cha biashara ya bangi kuwakamata wananchi na kuwaweka mahabusu bila kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Alisema kutokana na dosari hizo mbili, atazungumza na wahusika, akiwamo Waziri wa Maliasili na Utalii kwa upande wa tatizo linalohusiana na madai ya mazao ya misitu, pia atazungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro, ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Kuhusu uhaba wa maji, miundombinu na huduma za afya, Shaka alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeshatoa mafungu ya fedha katika kila sekta na miongoni mwa wanufaika ni Jimbo la Ushetu na Wilaya ya Kahama kwa ujumla.
"Kwa mfano kuhusu barabara, serikali imetoa Sh. milioni 500 kwa kila jimbo ili kuifanyia ukarabati barabara zake zipitike kwa ufanisi na kuwafungulia wananchi milango ya usafiri na usafirishaji.
"Kuhusu maji, nakuhakikishieni serikali imedhamiria na inatekeleza kwa vitendo kumtua mama ndoo kichwani. Imeshatoa Sh. milioni 400 kukamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya Jimbo la Ushetu na hiyo ni hatua muhimu kuhakikisha maji yanayotoka Ziwa Victoria yanawafikia wananchi wa Ushetu," alisema.
Mbunge wa Shinyanga Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Vijana, Ajira na Kazi, Patrobas Katambi, alisema serikali inatekeleza kwa vitendo mkakati wa kuwajengea uwezo wananchi wa kushiriki shughuli za kiuchumi.