KATIKA kuhakikisha kuwa wanakuwa na kikosi imara ambacho kitakuwa na uwezo wa kupambania makombe katika michuano wanayoshiriki, uongozi wa klabu ya Azam umefikia makubaliano ya kuimarisha mabenchi yao ya ufundi ya U17, na U20 kwa kuwaajiri makocha Mussa Rashid na Mohammed Badru.
Makocha hao wawili wote wamesaini mikataba ya miaka miwili kuitumikia Azam ambapo kocha Mussa Rashid atakuwa kocha wa U20, huku Mohammed Badru yeye akiwa kocha wa U17.
Kabla ya kupewa majukumu hayo Rashid alikuwa Kocha Mkuu wa timu ya African Sports, huku Badru yeye akiwahi kupita kwenye timu za Mtibwa Sugar, Gwambina na Malindi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema: “Katika kuhakikisha tunakuwa na kikosi kitakacholeta ushindani mkubwa hasa katika vita ya ubingwa katika michuano mbalimbali tutakayoshiriki, tumefikia makubaliano ya kuongeza nguvu katika mabenchi yetu ya ufundi ya timu za vijana chini ya miaka 20, na ile ya chini ya miaka 17.
“Kwenye kikosi cha U20 tumeingia mkataba na aliyekuwa kocha wa African Sports, Mussa Rashid na kwa upande wa U17 tumempa majukumu kocha, Mohammed Badru ambaye amewahi kuwa kocha wa Gwambina. Makocha hawa tumewapa malengo matatu makubwa, kwanza ni ishu ya kutwaa ubingwa katika mashindano yao, kupata wachezaji bora watakaopandishwa timu ya wakubwa na kufanya biashara ya wachezaji.”