Chama cha Demokrasia na Maendeleo, kimekanusha taarifa ya kwamba sababu ya kuzuiliwa kuingia Magereza kumuona Mwenyekiti wa Chama chao, Freeman Mbowe ni kutokana na hatua za kukabiliana na ugonjwa wa Korona.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi na wagombea waliokuwa kwenye msafara wa kwenda kumuona kiongozi wao Magereza, aliyekuwa Mgombea ubunge wa jimbo la Ulanga Celestine Simba, amesema sababu hizo hazina mashiko bali ni za kisiasa.
Bi. Simba leo Oktoba, 25, 2021 mbele ya wanahabari amesema kama ni njia za kujilinda walikuwa wameshajiandaa nazo ikiwa ni pamoja na uvaaji wa barakoa na vitakasa mikono.
Ameongeza kwamba ndani ya gereza la Ukonga hawaruhusu watu kuingia getini kama hawajajikinga kwa kuvaa barako hivyo kitendo cha wao kuwepo ndani ya geti inamaana tayari walikuwa wamekidhi masharti, na kusisitiza hata magereza wameweka maji tiririka kwa ajili ya wageni.
Hata hivyo Bi. Simba ameitaka magereza kutenda haki kwa Mbowe kwa kuruhusu kutembelewa kama ambavyo mahabusu wengine wanavyotembelewa.
Mwenyekiti wa CHADEMA Freema Aikael Mbowe, yupo Magereza tangu mwezi Julai akikabiliwa na mashtaka ya Ugaidi.
BY : Fatuma Muna