Chadema watuma salamu kwa Rais Samia, Jaji Mkuu, DPP




John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeomba kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan, ili kupata suluhu ya sintofahamu zinazojitokeza nchini kwenye masuala ya demokrasia, ikiwemo kesi inayomkabili Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Alhamisi, tarehe 21 Oktoba 2021 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya chama hicho, Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Mnyika amesema ni vyema Rais Samia akafanya mazungumzo na Chadema, ili kutafuta mustakabali wa demokrasia na maendeleo endelevu ya nchi.

“Tunasisitiza pamoja na kuminywa haki zetu, bado hatujafunga milango ya mazungumzo. Mwenyekiti Mbowe kabla ya kubambikiziwa kesi alimuandikia barua rais mwezi Aprili kwa ajili ya mazungumzo,”


 
“ Tunasisitiza ni vyema mazungumzo yakafanyika sababu yanahusu nchi,  sio tu kwenye kesi ya Mbowe, bali kwenye masuala makubwa kuhusu haki na maendeleo endelevu ya demokrasia,” amesema Mnyika.

Wito huo umekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano  mkoani Dar es Salaam, kutupilia mbali mapingamizi ya Mbowe na wenzake, dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adam Kasekwa.


Wakitaka yasitumike kama ushahidi wa jamhuri mahakamani hapo, wakidai yalichukuliwa kinyume cha sheria.


Mapingamizi hayo yalitupiliwa mbali na mahakama hiyo jana tarehe 20 Oktoba 2021, mbele ya Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani,  katika uamuzi wa kesi ndogo katika kesi ya msingi  ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka ya kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, inayomkabili Mbowe na wenzake watatu.

Mbali na Mbowe na Kasekwa, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Mohammed Abdillah Ling’wenya na Halfan Hassan Bwire, ambao wako mahabusu katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam, wakisubiri hatma ya kesi inayowakabili.

Mbali na ombi la kufanya mazungumzo na Rais Samia, Mnyika amemuomba kiongozi huyo nchi asahihishe kauli yake aliyoitoa kuhusu kesi hiyo, ya kwamba washtakiwa wenzake Mbowe wanatumikia kifungo, akidai kwamba inaathiri mwenendo wa kesi hiyo.


Rais Samia Suluhu Hassan
“Kwa sababu haya yanayoendelea ni matokeo ya kauli za rais ambazo ziliingilia uhuru wa mahakama, ni vizuri ajitokeze kusema ile kauli ya wenzake na Mbowe walifungwa , haikuwa kauli sahihi. Ili mahakama isiongozwe na kauli hiyo katika kufanya maamuzi,” amesema Mnyika.

Wakati huo huo, Mnyika ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, kuifuta kesi hiyo, akidai kuwa ni ya kisiasa.

Huku akimuomba Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, kuhakikisha mhimili anauongoza unatenda haki katika kesi hiyo.

“Mwito wetu ni kwamba makosa ambayo jaji mkuu aliyafanya yanaweza kurekebishika kwa kujirudi na kutambua umuhimu wa mahakama katika kutenda haki na kuhakikisha haki inatendeka. Wito wetu wa pili ni DPP kuifuta kesi,” amesema Mnyika.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad