Rais Samia atoa maagizo 5
RAIS Samia Suluhu, ametoa maagizio matano kwa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini ikiwamo kuoanisha mipango yao na vipaumbele na mipango ya kitaifa ya miaka mitano sambamba na Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDG).
Rais Samia ameyasema hayo leo mjini Dodoma, akihutubia Mkutano wa Mwaka wa Jukwaa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCONGO).
Kwanza Rais Samia ameyaagiza mashirika hayo kuusoma na kuutafsiri Mpango wa tatu wa Taifa wa miaka mitano katika kazi zao.
“Lengo ni kuutekeleza kwa pamoja serikali na ninyi ili twende kufanya kazi ambayo tumekusudia kwa haraka katika mpango huo.
“Pili natoa wito kuongeza uwazi na uwajibika kwenye utendaji wa kazi zenu, mwanzo nimeeleza kuwa kuna mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 11000 yaliyosajiliwa lakini yanayofanya kazi ni 4,663, hivyo kuna mashirika kama 7000 hayajulikani hayapo, yamekufa au vinginevyo.
“Hii ni kwa sababu mashirika mengi yanaanzishwa kwa ajenda iliyopo dunia kwa wakati ule, ulimwengu ukienda mazingira yatasajili mashirika ya mazingira. Ni kwa sababu wanajua fedha ipo pahali.
“Tuende kuendana na ajenda za ulimwengu mfano malengo endelevu na mpango wa serikali… tukienda hivyo wanaotoa fedha watakuelewa vizuri,” amesema
Aidha agizo la tatu, Rais Samia aliliotoa ni kuagiza mashirika ya ndani kupunguza utegemezi na kuagiza wizara ya afya kukaa na Baraza la mashirika hayo ili kutengeneza mpango mkakati ambao taasisi zitaweza kutafuta fedha zao na waweze kujitegemea.
“Nne, kama mnavyofahamu, nchi yetu ina utamaduni, mila na desturi zake hivyo basi natoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya kazi zinazoendana na tamaduni, mila, desturi na maadili ya kitanzania. Vilevile nitoe wito kwa baraza kuendelea kuwahimiza wanachama wenu kuzingatia sheria inayosimamia shughuli za mashirika haya.
“Lakini pia naomba mhamasishe watu wajitokeze kwa wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi ambayo itafanyika mwaka kesho,” amesema.