Watumiaji wanastahili kutupa simu zao za China na kujizuia kununua simu mpya, Waziri wa Ulinzi wa Lithuania ameonya.
Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Usalama wa Taifa wa Kimtandao, imesema imefanya majaribio ya simu za mkononi za 5G kutoka kwa watengenezaji wa China.
Na kudai kuwa simu ya Xiaomi ilikuwa imejumuishwa king’amuzi au kidhibiti wakati inatengenezwa kwa ndani huku simu nyingine aina ya Huawei ikiwa na mapungufu ya kiusalama.
Kampuni ya Huawei imesema kwamba hakuna data ya mtumiaji iliyoelekezwa kwengineko huku simu ya Xiaomi nayo ikisema kwamba sio kweli eti inachunguza mawasiliano ya watu.
“Mapendekezo yetu ni kwamba musinunue simu mpya za China, na pia muachane na zile ambazo tayari mumeshanunua haraka iwezekanavyo,” amesema Naibu Waziri wa Ulinzi Margiris Abukevicius.
Simu inayofanyiwa majaribio ya Xiaomi aina ya Mi 10T 5G ilipatikana kuwa programu ambayo inaweza kugundua na kudhibiti maneno ikiwemo “Mwachilieni huru Tibet”, “Maisha marefu uhuru wa Taiwan” au “vuguvugu la demokrasia”, ripoti hiyo imesema.
Iliangazia zaidi ya maneno 449 ambayo yanaweza kugunduliwa na programu za mfumo wa simu ya Xiaomi, pamoja na chaguo la kwanza la tovuti unayotaka kutumia.
Huko Ulaya, uwezo huu umelemazwa katika modeli hizi za simu, lakini ripoti zasema kwamba inaweza kuamirishwa kwa mbali wakati wowote.
“Vifaa vya simu ya Xiaomi havichunguzi mawasiliano kwa au kutoka kwa watumiaji wake,” msemaji aliiambia BBC. “Xiaomi haijawahi na haitawahi kuweka masharti au kuzuia tabia yoyote ya kibinafsi ya watumiaji wetu wa smartphone, kama vile kutafuta unachotaka, kupiga simu, kuingia kwenye wavuti unazotaka au matumizi ya programu ya mawasiliano ya mtu mwingine.”
Kampuni hiyo inatii kikamilifu masharti, aliongeza.
Utafiti pia uligundua kuwa kifaa cha Xiaomi kilikuwa kikihamisha data iliyosimbwa ya simu kwa seva huko Singapore.
“Hii ni muhimu sio kwa Lithuania tu bali kwa nchi zote zinazotumia vifaa vya simu vya Xiaomi,” Kituo hicho kilisema.
Watengenezaji wa simu za mkononi wameongeza kuwa umaarufu na bei yake rahisi, vimepelekea kuongezeka kwa mapato kwa asilimia 64 katika kipindi cha robo yake ya pili ya mapato ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Ripoti hiyo pia ilionyesha kasoro katika simu ya Huawei P40 5G, ambayo inaweka watumiaji katika hatari ya ukiukaji wa usalama wa mtandaoni.
“Programu rasmi ya Huawei inaelekeza watumiaji kwa maduka ya kielektroniki ya mtu mwingine ambapo baadhi ya programu zimetathminiwa na programu za kupambana na virusi kama hatari au kuambukizwa virusi,”taarifa ya pamoja ya Wizara ya Ulinzi ya Lithuania na Kituo chake cha Usalama wa Kimtandao kimesema.
Msemaji wa Huawei aliambia BBC kwamba inatii sheria na kanuni za nchi ambazo inafanya kazi, na inapeana kipaumbele kwa usalama wa kimtandao na faragha.
“Data hazitengenezwi nje ya kifaa cha Huawei,” ameongeza.
“Programu inakusanya tu na kuchakata data muhimu ili kuruhusu wateja wake kutafuta, kuweka na kudhibiti programu za watu wengine, kwa njia sawa na programu zingine.”
Huawei pia hufanya ukaguzi wa kiusalama ili kuhakikisha mtumiaji anapakua tu “programu ambazo ni salama,” alisema.
Mfano mwingine wa simu modeli ya 5G ya OnePlus pia ilichunguzwa na timu hiyo, lakini ilionekana kuwa haina matatizo.
Ripoti hiyo inakuja wakati kuna mvutano kati ya Lithuania na China unaozidi kuongezeka.
Mwezi uliopita, China ilitaka Lithuania imwondoe balozi wake kutoka Beijing na kusema itaondoa mjumbe wake kutoka Vilnius.
Mzozo huo ulianza wakati Taiwan ilitangaza kuwa ujumbe wake huko Lithuania utaitwa katika Ofisi ya Mwakilishi wa Taiwan.
Balozi zingine za Taiwan huko Ulaya na Marekani hutumia jina la mji mkuu wa nchi hiyo, Taipei, kukwepa kutaja kisiwa chenyewe, ambacho China inadai ni eneo lake.