Huwezi Amini..Polepole Aamua Kuwa Mwalimu wa Siasa Mtandaoni, Bashiru Amenyamaza Kimya



Mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole amegeuka mwalimu kupitia darasa la intaneti. Kupitia akaunti yake ya YouTube, hufundisha kitu anachokiita “Shule ya Uongozi”.

Wengi hutafsiri ‘mafunzo’ hayo ya uongozi kama vijembe kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa sehemu kubwa, ameamua kuweka safu mpya ya uongozi kwenye chama. Polepole yupo nje.

Polepole ni mbunge. Hata hivyo, haoni kama jukwaa lake bungeni linamtosha. Hivyo, anaamua kutumia intaneti kutema nyongo. Kuanzia kupinga chanjo ya Covid-19 mpaka kusimama kinyume na mpango wa kuhamisha wamachinga kwenye maeneo waliyovamia kipindi cha uongozi wa hayati, Dk John Magufuli.

Tafakari misimamo ya Polepole leo, kisha kumbuka msemo wa majigambo kwamba CCM ina wenyewe. Mwaka 2020, ungedhani hao wenyewe na Polepole yumo. Halafu ungeamini na Dk Bashiru Ally, aliyekuwa Katibu Mkuu CCM, naye ni mwenye chama. Siku hizi ni mbunge, ila yupo kimya!


Kama Polepole na Bashiru mwaka 2020, ndivyo mwaka 2015, ungeutafsiri msemo wa “CCM ina wenyewe” kwa kuwatazama Abdulrahman Kinana na Nape Nnauye.

CCM ina wenyewe, msemo huo bado upo hai? Hata baada ya kuwaona Kinana na Nape wakinung’unika kutotendewa haki na chama hicho kati ya mwaka 2018 na 2020? Sauti zao zikarekodiwa. Zikavuja. Nape akaomba msamaha kwa Dk Magufuli!

Jinsi Edward Lowassa alivyoingia kwenye siasa za nchi miaka ya 1970, akawa kijana wa chama, chini ya jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Tanganyika African National Union (Tanu Youth League), halafu UVCCM, kisha akapanda ngazi mbalimbali, ubunge, uwaziri mpaka waziri mkuu. Ungedhani mwaka 2015 angehamia Chadema na kugombea urais dhidi ya CCM?


Yusuf Makamba, kada asiyepaswa kutiliwa shaka wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Mtiifu wa chama tangu miaka ya 1970. Amepanda ngazi nyingi hadi ukatibu mkuu wa chama. Je, ungetarajia mwaka 2019, Makamba aungane na Kinana kulalamikia kutotendewa haki na CCM?

Uhai wa msemo huo, CCM ina wenyewe, unatokana na oksijeni ipi? Leo hii Daniel Chongolo na Shaka Hamdu Shaka, wanaweza kupaza sauti kumkalisha kimya Polepole. Miezi tisa iliyopita, ungedhani Polepole ndiye alikuwa na sauti kubwa ya kukisemea chama, baada ya Mwenyekiti, Dk Magufuli.

Tangu mwaka 1994, Augustino Mrema alipohama CCM na kujiunga na NCCR-Mageuzi, akila yamini kuwa akirejea CCM aitwe muongo na mnafiki, au mwaka 1995, Profesa Kigoma Malima alipoiacha Wizara ya Viwanda na Biashara na kuhamia NRA, hadi leo, bado kuna msemo CCM ina wenyewe?

Kama mwaka 2015, Kingunge Ngombale Mwiru, alipanda jukwaa la Chadema, akimfanyia kampeni Lowassa, halafu jukwaa la CCM, mhusika mkuu akiwa Dk Magufuli, ambaye ukirudi nyuma kabla ya mwaka 1995, humwoni akiwa na uzani wowote kwenye chama. Unaendeleaje kushikilia msemo wa CCM ina wenyewe? Ni msemo ambao ukiendelea kutumika basi ni makosa, kwani umechelewa kuondolewa. Chambilecho mwanasayansi nguli wa Marekani, Leon Kass, aliyesema kwamba msemo wa kwamba baiolojia ndio sayansi ya maisha yote, upo nje ya muda. CCM ina wenyewe ni msemo nje ya muda.


Badala yake, inapaswa kutamkwa kuwa CCM inakuwa na viongozi wapya wenye kushika hatamu kila baada ya muda. Hao ndio kwa kipindi husika husema na kuamua lolote. Na wakiondoka, hupoteza nguvu ya kufanya chochote, kisha huishia kulalamika.

Mwaka 1995, Mwenyekiti wa Kwanza wa Tanu na CCM, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliweka mezani kadi ya CCM na kuondoka kwenye chumba cha mkutano Dodoma, kwa kile alichoona kwamba aliyokuwa anataka yatokee hayakuwa yakisikilizwa. Nyerere akasema, CCM sio mama yake mzazi.

Hilo lilitokea baada ya Nyerere kutaka aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Dk John Malecela, ajiondoe au aondolewe kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM. Ilibidi Malecela akubali kujitoa kusudi hali ya chama iwe salama.

Je, baada ya Nyerere, aliyekuwa na kadi namba moja ya CCM, kutamka chama hicho si mama yake mzazi, msemo wa kwamba CCM ina wenyewe kwenu bado una nguvu? Vipi, Malecela aliyepata pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara kwa miaka 15, kung’olewa mapema kwenye uteuzi wa mgombea urais mwaka 1995 na 2005?


Mwaka 2010, Malecela alivyoshindwa na Livingstone Lusinde, kwenye kura za maoni CCM, kuwania jimbo la Mtera (siku hizi linaitwa Mvumi). Kila hesabu utakayopiga, utabaini kuwa CCM haina mwenye nayo.

Leo, Mwenyekiti ni Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye historia inaonesha kuwa kabla ya mwaka 2000, hakuwa na utambulisho wowote katika vikao vya chama. Katibu Mkuu ni Chongolo, ambaye ukimrudisha nyuma mpaka mwaka 2015, utamkuta alikuwa msaidizi wa Nape, alipokuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM.

Kama mwaka 2012 Frederick Sumaye, Waziri Mkuu wa Saba wa Tanzania, alilalamika kuchezewa rafu kwenye uchaguzi wa chama, alipokuwa anagombea ujumbe wa Halmashauri Kuu CCM, una ubavu gani leo kusema CCM ina wenyewe? Swali, akina nani hao? Waliokuwepo jana, leo hawana ubavu. Wa leo, kesho ikifika hawatakuwa na chao.

Ndio maana Bashiru, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, leo ni mbunge asiye na cheo chochote bungeni. Waingereza wanaita backbencher MP, yaani mbunge wa dawati la nyuma. Sawa na Polepole, aliyekuwa na sauti kali pindi alipokuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi.

Siku hizi Polepole analalamika mitandaoni, Chongolo, Shaka na Katibu Mkuu UVCCM, Kenani Kihongosi, wanamwambia anyamaze, vinginevyo atachukuliwa hatua. Upande wa pili Bashiru yupo kimya. Ni kwa sababu CCM haina wenyewe. Maana kila zama zinakuwa na wenyewe wapya. CCM haina wenyewe wa kudumu.


CCM mwanzo wake ni Julai 5, 1954, wakati huo kikiwa na jina la Tanganyika African National Union (Tanu) na Februari 5, 1957, Afro-Shiraz Party (ASP). Februari 5, 1977, Tanu na ASP vikaungana kupata CCM. Hivyo, CCM mizizi yake ina zaidi ya miaka 67. Wengi waliopo, wamekuta ipo, inaongoza, je, nani mwenye CCM?

Mwananchi

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad