Kada Kindaki Ndaki wa Chadema arudi CCM mbele ya Rais Samia, aomba kazi





ALIYEWAHI kuwa Diwani wa Sombetini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ally Bananga, ametangaza kurejea katika chama tawala cha Mapinduzi (CCM), mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Bananga aliyewahi kugombea uenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini na kushindwa na Godbless Lema ametangaza uamuzi huo leo Jumapili, tarehe 17 Oktoba 2021, katika mkutano wa hadhara wa Rais Samia, mkoani Arusha, Uwanja wa Amri Abeid.

Mwanasiasa huyo amesema ameamua kuvunja msimamo wake wa kutorejea CCM, baada ya kuridhishwa na utendaji wa Rais Samia.

“Moyo wangu umerudi CCM na umerudi sababu wako walinishawishi nilikataa siku zote, lakini sasa nimeamua mwenyewe kurudi CCM. Nimerudi kwa moyo wangu kilichonisukuma ni haya yanayoendelea hasa ujenzi wa Hospitali ya Jiji la Arusha,” amesema Bananga.


Bananga ameiomba radhi CCM, na kuomba apewe kazi ya kufanya ikiwemo kumsaidia Rais Samia katika kunadi utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa 2021.




“Niombe radhi kwa yote magumu niliyosema, sahauni sasa mko na mwanaCCM sana. Niwaahidi utumishi uliotuka nipeni kazi ya kufanya, Chongolo (Katibu Mkuu CCM, Daniel Chongolo) na Shaka (Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Shaka Hamdu Shaka), lililogumu nipeni,” amesema Bananga.

Amesema, yeye amemuoa mnyamwezi, Hawa Mwaifunga, mbunge wa viti maalum asiyekuwa na chama bungeni baada ya kufukuzwa Chadema. Hawa ni miongoni mwa wabunge 19 waliofukuzwa Chadema.

Bananga amesema, tangu Rais Samia aingie madarakani nchi imepumua.


Hawa Mwaifunga, Mbunge wa viti Maalum
“Nawaomba wanaCCM wote mliopo hapa niruhususni kuwa miongoni mwenu nisaidieni na ninyi kuinadi ilani ya CCM, lakini kubwa kusaidiana na mama yetu kueleza mazuri yanayofanyika kwa mustakabali mzima wa maendeleo ya Tanzania nzima,” amesema Bananga na kuongeza:

“Ambapo kwa miezi sita nchi inatabasamu, inapumua. Mama uliyofanya kwetu kama wapinzani tukatae tu, lakini sitaki kuwa na nongwa mama unayaweza ya sasa, unayaweza yajayo.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad