Kagere Akabidhiwa ufalme Simba SC




BAADA ya Ijumaa iliyopita mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere kufunga bao pekee kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, ametoa kauli ya kumkabidhi ufalme Mnyarwanda huyo.


Kagere ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara misimu miwili mfululizo 2018/19 na 2019/20, alifunga bao hilo la kwanza kwa Simba msimu huu baada ya timu hiyo kucheza mechi mbili bila ya kufunga kwenye Ngao ya Jamii na mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara.


Mshambuliaji huyo anayetajwa kutumia nguvu na akili kuwamaliza wapinzani, aliimalizia vema pasi ya kichwa na Chris Mugalu na kumchambua kipa wa Dodoma Jiji akiuweka mpira kimiani.


Gomes ameliambia Spoti Xtra kwamba, tayari ameusoma ushindani uliopo ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu, hivyo kufuatia namna ya uchezaji wa timu pinzani, ameahidi kuhakikisha anatumia washambuliaji wenye nguvu kama ilivyo kwa Kagere ili kuendana na hali ya ushindani.


“Tulianza kwa kusuasua kutokana na kutoijua ligi ya mwaka huu ndiyo maana tulipata shida kubwa mbele ya Biashara United, ila mchezo wetu na Dodoma Jiji, pamoja na kupata pointi tatu, pia tumejua mwenendo wa ligi kwa jumla, hivyo nitahakikisha natumia wachezaji wenye nguvu kwenye michezo ijayo.

 

“Nafahamu vizuri uchezaji wa Polisi Tanzania ambao tutakutana nao katika mchezo ujao, nitahakikisha nawaandaa zaidi nyota wangu kupambana kwa nguvu ili kulinda hali hii ya kujikuta tunatumia nguvu nyingi zaidi kupata ushindi, maana wapinzani wetu wanatumia nguvu ili kutubana,” alisema Gomes.

KAGERE AFIKISHA MABAO 59 BONGO

Bao lake dhidi ya Dodoma Jiji, limemfanya Meddie Kagere kufikisha mabao 59 ndani ya Ligi Kuu Bara akiwa amecheza misimu minne sasa.

Nyota huyo ambaye aliibuka Simba msimu wa 2018/19 akitokea Gor Mahia ya Kenya, amekuwa akitajwa kuwa moja ya washambuliaji hatari akibeba Tuzo ya Ufungaji Bora mara mbili mfululizo ndani ya Ligi Kuu Bara.

Msimu wa kwanza 2018/19 alitupia mabao 23 na kuwa kinara, kisha msimu wa 2019/20 akawa tena kinara akifunga mabao 22, huku msimu wa tatu 2020/21 akifunga mabao 13 akishika nafasi ya nne nyuma ya kinara John Bocco aliyefunga mabao 16. Juu yake walikuwa Chris Mugalu (15) na Prince Dube (14).

JOEL THOMAS, Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad