Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Hashim Issa (63), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashitaka mawili likiwemo la kuchapisha taarifa za uchochezi.
Mzee Issa amesomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu ambapo amesomewa na wakili wa serikali, Yusuph Aboud ambapo imedaiwa mshitakiwa huyo alitenda makosa hayo Oktoba 1, mwaka huu mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika shitaka la kwanza mshitakiwa huyo akiwa eneo hilo alichapisha taarifa ya uongo kwa njia ya kompyuta na kusambaza katika mtandao wa YouTube kwa lengo la kumchafua na kumdharilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro.
Imeelezwa mshitakiwa huyo alichapisha taarifa kuwa ‘IGP Sirro ni gaidi namba moja hapa nchini Tanzania na fisadi’ wakati akijua si kweli.
Katika shitaka la pili, nikwamba katika tarehe na eneo hilo, mshitakiwa huyo alichapisha taarifa ya uchochezi kwa lengo la kutengeneza chuki kwa wananchi wa Tanzania dhidi ya IGP Sirro kuwa ‘IGP Sirro ni gaidi namba moja hapa nchini Tanzania na fisadi’ wakati si kweli.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo upande wa mashitaka ulidai,upelelezi wa kesi hiyo upo katika hatua za mwisho hivyo wapangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu amekubali ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 28 mwaka huu.
Mshitakiwa huyo amefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya kura au cha taifa watakaosaini bondi ya sh milioni tatu kila mmoja.