Kitendawili cha Tundu Lissu, Godbless Lema Kurejea Tanzania





Wakati Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema akidokeza mpango wake wa kurejea nchini kuendelea na siasa, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu amesema sababu zilizomfanya aondoke hazijaondoka bado zipo.


Kurejea kwa viongozi hao ambako kumeibuka mtandaoni huenda ukakiongezea nguvu chama hicho ambacho kwa sasa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe yuko rumande akiendelea na kesi yake inayomhusisha makosa ya ugaidi.



Kutokuwepo viongozi hao mara kadhaa umetajwa kupunguza hamasa ya siasa kwa chama kikuu cha upinzani nchini na kusitisha programu zake kadhaa.



Hakikisho la Lema

Akizungumza juzi katika mitandao ya jamii, Lema aliyeondoka nchini baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alisema anatafakari kufanya uamuzi wa kurejea Tanzania kuungana na ndugu zake, akisema majadiliano kuhusu hatua hiyo anayaanza hivi sasa.



“Nafanya uamuzi wa kuwepo Tanzania lini? Naanza sasa majadiliano na Mungu, familia na chama changu ili kufanya kazi pamoja. Nahitaji kuwa uwanjani (Tanzania) kuliko wakati wowote ule, nitakuwa tayari kukabiliana na matokeo yoyote,” alisema Lema.



Lema ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alieleza hayo katika mtandao wa Club House unaowakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili na kutoa maoni kuhusu mada inayowekwa mezani katika siku husika.



Kwa sasa Lema ambaye aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini anaishia nchini Canada alikopata hadhi ya ukimbizi wa kisiasa akitokea Nairobi, Kenya.



Katika mtandao huo, Lema alisema, “nafikiria nahitaji kumuona mwenyekiti (Freeman Mbowe) jela, akiwa mahabusu au mahakamani. Nahitaji kumtia matumaini, nahitaji vitu vingi kuhusu nyumbani, nipo tayari kwa lolote kabisa,” alisema Lema.



Lema aliwataka viongozi wa Chadema kusimama imara katika usimamizi wa kesi ya Mbowe, akisema mazingira ya kesi hiyo ni magumu.



Wakati, Lema akisema hayo, kiongozi mwenzake anayeishi nchini Ubelgiji Tundu Lissu alisema sababu zilizomkimbiza Tanzania kwenda ughaibuni bado hazijabadilika.



Lissu aliondoka nchini kwa mara ya kwanza Septemba 7, 2017 na kuelekea Nairobi, Kenya akiwa mahututi, baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana jijini Dodoma.



Mwaka 2018 alihamishiwa nchini Ubeligiji kwa matibabu zaidi hadi mwaka 2020 aliporejea nchini na kugombea urais, kabla ya kurejea tena Ubelgiji akidai kutishiwa maisha yake.



Akizungumzia hoja zilizoibuka mtandaoni baada ya mchungaji mmoja kuonekana akimkaribisha nyumbani, Lissu alisema “mtandaoni kuna Tundu Lissu wengi, huyo anayeelezwa na pastor (jina tunalihifadhi kwa sababu hatukumpata), sio yule Tundu Lissu aliyeko uhamishoni.



Alipotakiwa kufafanua kauli yake, Lissu alisema: “Sababu zilizonikimbiza Tanzania hazijabadilika. Wauaji bado wako huru mitaani na hakuna mpango wa kuwatafuta na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria.’’
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad