Jaji Mustapha Siyani aliyekuwa akiendesha kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake amejitoka kuendesha kesi hiyo leo Jumatano, Oktoba 20, 2021, kwa kile alichodai kuwa kwa sababu ya uwingi wa majukumu unaotokana na uteuzi alioupata hivi karibuni.
Jaji Siyani ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais Samia Suluhu na kuapishwa kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ametangaza uamuzi huo muda mfupi baada ya kutoa maamuzi ya kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya Mbowe na kutupilia mbali mapingamizi ya Mbowe.
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imetupilia mbali mapingamizi mawili yaliyowasilishwa na upande wa utetezi.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Mustapha Siyani ambaye kwa sasa ni Jaji Kiongozi, amesema mapingamizi yote mawili yamekosa mashiko, ambapo katika pingamizi la kwanza, mahakama imejiridhisha kwamba maelezo yalichukuliwa ndani ya saa nne zinazoruhusiwa kisheria na katika pingamizi la pili, mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa ‘Adamoo’ alitoa maelezo ya onyo kwa ridhaa yake.