KLABU ya Soka ya Yanga, imepigwa faini ya Dola za kimarekani 5,000 sawa na Sh. 11 milioni za kitanzania, na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), baada ya kukutwa na makosa mawili ya utovu wa nidhamu, kwenye mchezo wake wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Shirikisho hilo lilitoa adhabu hizo jana, kupitia kamati ya nidhamu mara baada ya kupitia malalamiko mbalimbali yaliwasilishwa ndani ya Shirikisho hilo.
Adhabu hiyo kwa Yanga, imekuja kufuatia malalamiko yaliyopelekwa na klabu ya Rivers United ya kufanyiwa fujo baadhi ya viongozi wao walipokuja kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF ilieleza kuwa, baada ya kupokea malalamiko hayo, waliwatumia Yanga, kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lakini hawakupata mrejesho wowote na kuamua kuwachukulia hatua hizo.
Katika mchezo wa hatua hiyo, Rivers United ilifanikiwa kuiondosha Yanga kwenye michuano hiyo, kwa jumla ya mabao 2-0, katika michezo yote miwili.
Aidha kosa lingine lililowaghalimu Yanga kupigwa faini hiyo, ni kuingiza baadhi ya watazamaji kwenye huo wakiwa nyumbani dhidi ya Rivers United, huku kukiwa na katazo la kuingiza mashabiki kwenye mchezo huo.