KOCHA Mkuu wa Simba raia wa Ufaransa, Didier Gomes Da Rosa, ameendelea kuwafanyia umafia wa kutosha wapinzani wake, Jwaneng Galaxy FC ya Botswana, baada ya kuwaingiza mashushu kwenye mazoezi yao na kuiba mbinu zao.
Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza utakaozikutanisha timu hizo Oktoba 17, mwaka huu nchini Botswana kabla ya kurudiana Dar, Oktoba 24, mwaka huu.
Simba ambayo kesho Ijumaa inatarajiwa kuelekea Botswana, tayari imetuma watu wao mapema kufika nchini humo na kuweka mambo sawa.
Chanzo chetu kutoka nchini Botswana, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, Gomes kwa kushirikiana na mtaalam wa mambo ya tathmini za wachezaji, Culvin Mavhunga, wamehakikisha wanawapenyeza mashushu kwenye mazoezi ya Jwaneng Galaxy na kufanikiwa kupata mbinu zao.
“Tunamshukuru Mungu kwa uwezo wake ameendelea kutulinda tangu tuje huku, tupo hapa Botswana kuhakikisha tunafanya kila liwezekanalo ili kikosi chetu kikifika kisipate tabu.
“Mbali na hivyo, kocha naye ameendelea kutuagiza kuhakikisha tunampatia kila anachokihitaji kwa wapinzani wetu.
“Kama mambo yataenda hivi bila shaka tutatoka na matokeo mazuri kwenye mechi hiyo ya Jumapili, maana leo (Juzi Jumanne), kuna baadhi ya watu wetu waliingia mazoezini kumsaidia kocha kupata baadhi ya mbinu za wapinzani wetu jambo ambalo limefanikiwa.
“Kwa sasa kila kitu tunamuachia kocha ili aweze kututengenezea mbinu sahihi za ushindi.
“Kocha mwenyewe ameonekana kukubaliana na kazi inavyofanyika kuhakikisha ushindi unapatikana,” kilisema chanzo hicho.
WACHEZAJI WAPIMWA COVID-19
Katika kujiandaa na safari yao, jana asubuhi wachezaji wote wa Simba walifanyiwa vipimo vya Covid -19.
Simba wamechukua uamuzi huo ili kuepuka hujuma za wapinzani wao ambapo kumekuwa na taarifa kwamba timu zinapokwenda kucheza ugenini kipindi hiki, zinakumbana na kupewa majibu feki ya vipimo vya ugonjwa huo ili tu kuzuia baadhi ya wachezaji muhimu wasicheze.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema vipimo hivyo vimefanyika katika Hospitali ya Muhimbili, Dar.
“Wachezaji wetu pamoja benchi la ufundi leo (jana) asubuhi wamepimwa Covid-19 tayari kwa maandalizi ya safari kuelekea Botswana.
“Kupima Covid-19 kabla ya safari kutoka nchi moja hadi nyingine ni utaratibu uliowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.
“Kikosi kinaelekea Botswana tayari kwa mchezo wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galax utakaopigwa Jumapili, Oktoba 17.
“Wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa wameanza kurejea huku wale waliokuwa Taifa Stars wakifanya mazoezi na wenzao tangu jana (Jumanne).”
MUSA MATEJA NA WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam