ACHANA na saa aina ya Rolex aliyonunua wiki hii nchini Marekani yenye thamani ya shilingi milioni 69 za Kitanzania, siri nzito imevuja katika manunuzi makubwa ya magari matatu ya kifahari yaliyofanywa miezi mitatu iliyopita na supastaa wa muziki barani Afrika, Nasibu Abdul almaarufu Diamond Platnumz kuwa ni hasara tupu, Gazeti la IJUMAA limedokezwa.
Gazeti hili limefika nyumbani kwa Diamond au Mondi maeneo ya Mbezi-Beach, Kwazena jijini Dar na kuyashuhudia magari hayo yakiwa yameegeshwa tu bila kutumika.
MAGARI HAYATUMIKI
Kwa mujibu wa waliokutwa nyumbani hapo wakiwemo walinzi, Mondi au Baba T ambaye kwa sasa yupo kwenye ziara ya kimuziki nchini Marekani, kwa muda mrefu tangu ayanunue magari hayo amekuwa hayatumii, badala yake amekuwa akiendelea kutumia yale ya zamani kama Toyoya Land Cruiser V8 (nyeusi).
Hadi sasa, Mondi kwenye ‘parking’ yake kuna magari ya kifahari na ya bei mbaya aina ya Cadillac Escalade (yapo mawili), Rolls Royce, Toyota Land Cruiser V8 (yapo mawili) Toyota Prado pamoja na BMW X6; lile la bluu lenye jina la Platnumz balada ya namba ya usajili.
MAGARI YA BILIONI 3
Hata hivyo, magari matatu ya Mondi ambayo yanatajwa kumgharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu za Kitanzania na sasa anashindwa kuyatumia ni Cadillac Escalade (mawili) na Rolls Royce Cullinan ambayo ameishia kurekodia matangazo ya shoo zake za Marekani.
WACHUMI WAINGILIA KATI
Baadhi ya wachumi waliozungumza na Gazeti la IJUMAA, wameingilia kati ishu hiyo na kushauri vijana kuwa makini mno wanapofanya manunuzi ya vitu vya kifahari ambavyo ni liabilities (yaani vinamuingizia mtu gharama) badala yake wanunue assets (yaani vitu vinavyoingiza faida).
Wachumi hao wanasema kuwa, kwa namna yoyote, kwa kuwa magari hayo ya Mondi hayazalishi, bali yatakuwa yanaingiza hasara tupu kwa sababu hayawekwi mafuta ya kibaba na yanahitaji ‘sevisi’ za gharama kubwa.
UFAHARI TU?
Wanasema kuwa, kama Mondi alinunua magari hayo kwa ajili ya kuonesha ufahari tu, basi ajue kwamba muda siyo mrefu mbwembwe hizo zitakwisha na zinaweza kumuacha pabaya kiuchumi na atakuwa anajilaumu kwamba huwenda angenunua gari kama Range Rover tu ingetosha.
NGUMU KUUZIKA
Kwa mujibu wa wachumi hao, aina ya magari hayo matatu aliyonunua Mondi au Chibu Dangote huwa hayana thamani baada ya kununuliwa na huwa ni ngumu mno kuyauza kwani siyo rahisi kupata mnunuzi endapo atataka kuyauza.
Wamesema kuwa, na kama atataka kuyauza, basi hawezi kupata pesa nzuri kama aliyonunulia hivyo lazima tu aingie hasara.
KWA AJILI YA BIASHARA?
Wengine walikwenda mbali zaidi na kusema kuwa, kama magari hayo aliyanunua kwa ajili ya kuyafanyia biashara f’lani, basi biashara hiyo inaweza kuwa ngumu vilevile kwa watu wengi kuyaogopa kwamba ni ya gharama kubwa.
NINI CHA KUFANYA?
Hata hivyo, baadhi ya wataalam hao wanashauri nini cha kufanya juu ya magari hayo ili kukwepa hasara kuwa ni pamoja na kuwakodishia wasanii wenzake kwa ajili ya appearance (kutokea kwenye shughuli maalum au shoo) au kwa maharusi ambao watapenda kuvimba nayo kwenye siku yao kubwa ya kufunga ndoa.
“Mimi naamini wapo watu ambao watataka kuyatumia hasa maharusi. Lakini kuendelea kuyaweka kwenye maegesho na hata akiyafunika na maturubai, lazima atakuja kulia tu kutokana na hasara atakayoipata,” anasema Innocent Mosha ambaye ni mtaalam wa masuala ya uchumi nchini Tanzania na kuongeza;
“Tajiri mmoja wa Marekani aitwaye Robert Kiyosaki alipata kufundisha kuwa assets ni vitu vinavyokuingizia pesa, liabilities vinatoa pesa mfukoni, ukitaka kuwa tajiri, assets ziwe nyingi kuliko liabilities na hicho ndicho Diamond alichopaswa kukizingatia.”