Mahakama kutoa uamuzi kesi ya Mbowe kesho



MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa (Mahakama ya Mafisadi) kesho itatoa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Uamuzi huo ulipangwa kutolewa leo, lakini utatolewa kesho kwa kuwa leo ni mapumziko ya maadhimisho ya Sikukuu ya Maulid. Washitakiwa wengine ni Khalfan Bwire na Mohamed Ling'wenya.

Katika kesi hiyo inayoendeshwa na Jaji Mustapha Siyani, upande wa utetezi ulifungua kesi ndogo kupinga kupokelewa kwa maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa pili katika kesi ya msingi, Adam Kasekwa kwa madai kuwa kabla  na wakati wa kuchukuliwa maelezo hayo aliteswa na pia yalichukuliwa nje ya muda jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Kesi hiyo ndogo ilikuwa ni matokeo ya shahidi wa kwanza katika kesi ya msingi, Ramadhani Kingai kuiomba mahakama ipokee maelezo ya onyo ya mshitakiwa Kasekwa ili yawe moja ya vielelezo katika mwenendo wa kesi hiyo.

Ombi hilo lilipingwa na upande wa utetezi na ukaomba mahakama ianze kusikiliza kesi hiyo ndogo.

Upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi watatu na baadaye upande wa utetezi nao uliwasilisha mashahidi watatu.

Baada ya takribani wiki mbili za kusikiliza kesi hiyo ndogo, Septemba 29 mwaka huu ushahidi wa pande zote mbili ulikamilika na kufungwa.

Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka unawakilishwa na mawakili wa serikali waandamizi, Pius Hilla, Robert Kidando, Abdallah Chavula, Nassoro Katuga, Esther Martin na Janetreza Kitali.

Upande wa utetezi unawakilishwa na Peter Kibatala akisaidiana na Rwekama Rwekiza, John Malya, Frederick Kihwello, Selemani Makauka, Michael Lugina, Iddi Msawanga, Jebra Kambole, Cisty Aloyce na Maria Mushi.

Katika kesi ya msingi, Mbowe aliunganishwa na wenzake watatu ambao walisomewa mashitaka kabla yake.

Mbowe anakabiliwa na mashitaka mawili likiwamo la kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi.

Mbowe anadaiwa kula njama kwa dhamira ya kutenda kosa chini ya Sheria ya Ugaidi na katika shitaka la pili inadaiwa kati ya Mei na Agosti, mwaka jana akiwa katika hoteli ya Aisha iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro alitoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad