Mahakama yatupa kesi ya kupinga CAG kuhojiwa na Bunge





 Mahakama Kuu ya Tanzania imetupilia mbali kesi ya kikatiba ya kupinga kuhojiwa aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka kwa tuhuma za kuliita Bunge la Tanzania dhaifu.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, lililooongozwa na Jaji Dk Benhajj Masoud, akishirikiana na majaji Elinaza Luvanda na Yose Mlyambina.


Katika uamuzi huo ulioandikwa na Jaji Luvanda kwa niaba ya jopo hilo, wa Oktoba 7, mwaka huu ambao Mwananchi limeuona nakala yake leo Jumatatu, Oktoba 25, 2021, mahakama hiyo imeitupilia mbali kesi hiyo ikisema kuwa haina mashiko ya kisheria na kwamba mdai hakuwa na hoja za msingi.

Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 01 la mwaka 2019, lilifunguliwa na Kiongozi wa Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe Mahakama Kuu, Masjala Kuu, dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Katika shauri hilo Zitto alikuwa akipinga uamuzi wa Spika Ndugai kumtaka, CAG Profesa Assad kufika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa kutokana na kauli yake aliyoitoa wakati akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa, nchini Marekani Januari 7, 2019, kuwa Bunge la Tanzania ni dhaifu.


Zitto ambaye alikuwa akiwakilishwa na wakili wa kujitegemea Jebra Kambole alikuwa akidai kuwa kitendo cha Spika kumuita CAG kuhojiwa kwenye kamati ya Bunge kwa kauli hiyo hakikuwa halali na kwamba kilikuwa kinyume cha Katiba.


Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo wakili wa Zitto, Kambole alidai kuwa CAG alikuwa akitoa maoni yake kuhusiana na majukumu yake kama CAG nchini Tanzania na kwamba alikuwa akitumia uhuru wake wa kujieleza unaolindwa na Katiba ya nchi na mikataba ya Kimataifa.

Alisisitiza kuwa mamlaka hayo ya Bunge kumuita mtu yeyote chini ya Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki ya Bunge yana ukomo kwa kuwa kuna baadhi ya watu wana kinga ya kisheria, akiwemo CAG ambaye alidai kuwa halazimiki kutimiza maelekezo ya mtu au idara yoyote ya Serikali.


Badala yake wakili Kambole alidai kuwa taasisi yenye mamlaka pekee ya kuhoji jambo lolote linalofanywa na CAG ni Mahakama na si Kamati ya Bunge.

Mahakama katika uamuzi baada ya kurejea Sheria na Kanuni za Bunge nayo imekubalinana na hoja za Serikali kupitia kwa Wakili Mkuu wa Serikali (Solicitor General-SG), Gabriel Malata ikisema kuwa Bunge au Kamati ya Bunge ina mamlaka ya kumtaka mtu yeyote kufika mbele yake.


“Ni kweli kwamba CAG analindwa chini ya masharti ya Ibara ya 143(6) ya Katiba. Hata hivyo haki hiyo hapa ina mpaka kwa kumlinda CAG wakati tu anatekeleza majukumu yake.” imesema mahakama hiyo katika uamuzi huo, kwa tafsiri isiyo rasmi na kunukuu Ibara hiyo ndogo ya 6 ya Ibara ya 143 ya Katiba.


Mahakama hiyo imesema kuwa ingekubali kuwa CAG alikuwa anatoa maoni yake katika dhana ya uhuru wa kujieleza, lakini ikasema kuwa kipimo cha hilo ni kama kauli hiyo aliyoitoa wakati wa mahojiano hayo ilikuwa inahusiana na utendaji kazi wake kama CAG nchini Tanzania.


“Tunafahamu kwamba mahojiano yalihusiana na taarifa za CAG na mapendekezo yanayotolewa humo. Lakini hakuna mahali popote paliposemwa kwamba madai ya udhaifu wa Bunge ni miongoni mwa mapendekezo yake, ili kuwa na haki hiyo.” imesema mahakama hiyo.


Imesema kuwa kama taarifa ya CAG ingekuwa na maoni hayo miongoni mwa mengine kuwa Bunge ni dhaifu, basi kauli ya CAG ingekuwa imelindwa na Ibara ya 143 (6) ya Katiba.

 


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad