Majanga; Koffi Olomide ahukumiwa miaka nane jela kwa ubakaji





NYOTA wa muziki wa rhumba na soukous ambao ni maarufu zaidi Barani Afrika, Koffi Olomidé amekumbwa na majanga mengine huko nchini Ufaransa baada ya kuhukumiwa kwenda jela miaka nane kutokana na makosa ya ubakaji na unyanyasi kingono aliowatendea wanenguaji wake wanne. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Hukumu ya kesi hiyo iliyopewa jina la ‘Le Grand Mopao’ imetolewa mapema wiki hii tarehe 25 Oktoba, 2021 na Mahakama ya Rufaa ya Versailles jijini Paris nchini humo.

Koffi ambaye sasa makazi yake yapo huko nchini Ufaransa alikuwa anashtakiwa kwa kuwadhulumu kingono na kuwabaka wanenguaji wanne wa kike waliokuwa wakicheza dansi wakati walipofanya naye kazi kwenye matamasha nchini Ufaransa kati ya mwaka 2002 na 2006.

Hukumu hiyo ya kwanza kutokana na mashtaka, hayo, inasubiri mkazo wa hukumu ya pili ambayo itatolewa baadae mwezi Disemba mwaka huu kabla ya kuanza kutumikia adhabu hiyo.


 
Koffi mwenye umri wa miaka 65, ambaye jina lake halisi la Antoine Agbepa Mumba licha ya kutokuwepo mahakamani alihojiwa mwaka 2012 kwa tuhuma hizohizo za ubakaji wa wacheza dansi wanne.

Baadaye mwaka 2019, Mahakama ya hiyo ya Nanterre ilimhukumu kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kumnyanyasa kingono mmoja wa dansa wake ambaye alikuwa mtoto wa miaka 15 na kuamriwa kulipa faini ya euro 5,000 sawa na Sh milioni 13.

Pia mahakama hiyo ilimuamuru kulipa faini sawa na hiyo kwa kuwasaidia wanawake watatu kuingia nchini Ufaransa kinyume cha sheria.


Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo Wizara ya Utawala nchini humo ambayo ilikuwa imeomba afungwe kwa miaka saba, ilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Koffi Olomide ambaye mara kadhaa amekuwa akisema hadharani kuwa ananyanyaswa, anaendelea kukanusha tuhuma za ubakaji.

Mwaka wa 2019, aliiambia TV5 Monde kwamba “Ninatumaini kuwa siku moja wanawake hawa watakuja na kusema kwamba wamedanganya kuhusu madai hayo.”

Wanawake hao wanamshutumu kwa kuwapa hifadhi katika nyumba iliyo karibu na nyumba yake huko jijini Paris na kuwalazimisha kufanya naye mapenzi ili baadhi yao waweze kuendelea kukaa hapo.


 
Mbele ya majaji, Koffi alikanusha mashtaka hayo waziwazi, akidai kuwa wanawake hao walisafiri kwenda na Ufaransa na kutoka Kongo na wakati mwingine walidai wasindikizwe”.

Koffi alithibitisha kuwa ana haki ya kuwasimamia walipoondoka kurejea Kongo, ili kuhakikisha kuwa hawatoroki Ufaransa kutokana na kazi waliyokuwa nayo.

Amesema madai hayo yametungwa na wanawake hao wanne wanaotafuta namna ya kuendelea kuishi Ufaransa.

Akingumzia namna wasichana hao walivyotoroka nyumba waliyokuwa wakiishi, Koffi amesema, “Hiyo ni sinema tu… muda wao wa kurudi Kongo ulikuwa unakaribia na walijua kabisa kwamba wanatakiwa kurudi Kongo, kwa hiyo walitoroka ili kutafuta namna ya kuendelea kukaa Ufaransa kwa gharama yoyote,” alisema.


Wanawake hao wanasema walishindwa kurejea Kongo kwa kuhofia kulipizwa kisasi.

Koffi Olomide pia alikanusha madai ya ubakaji wa wanawake hao ambao walisema wakati fulani aliwaalika hotelini na kwenye studio ya muziki kisha kuwalazimisha kufanya naye mapenzi.

Koffi alisema, “hapana, sijawahi kuwa peke yangu na hawa wasichana, unawezaje kufanya mapenzi studio? Siwezi kuwafikia!

“Hakuna ushahidi wa kuunga mkono madai yaliyotolewa na washtaki hawa.”

Mahakama ilisema itatangaza uamuzi wa mwisho tarehe 13 Desemba mwaka huu.


 
Koffi ana kesi nyingine zinazomkabili

Mwaka 2012 alifungwa gerezani kwa kipindi cha miezi mitatu huko Kongo baada ya kushtakiwa kumpiga na kumuumiza mtayarishaji wa muziki.

Mwaka 2018, Serikali ya Zambia ilimshtaki kwa kumuacha mpiga picha wake

Mwaka 2016, alikamatwa jijini Nairobi nchini Kenya na kurudishwa kwao baada ya kumpiga mnenguaji wake wakati anawasili Kenya kufanya tamasha.

Mwaka 2008, alishutumiwa kwa kumpiga mpiga picha wa kituo cha televisheni RTGA kilichopo Kongo na kuharibu kamera yake lakini lakini baadae walipatana nje ya kesi.

Koffi alitarajiwa kuwa na tamasha tarehe 13 Februari mwaka huu jijini Paris katika ukumbi wa La Defense Arena lakini tamasha hilo lilisogezwa mbele hadi tarehe 27 Novemba mwaka huu kutokana na masharti ya janga la Corona.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad