Mambo 5 yanayosababisha Biashara nyingi za Wanawake kufa





Hivi leo wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahi na kufanyia kazi fursa mbalimbali. Fursa hizo ni pamoja na uwekezaji katika biashara ndogo na za kati. Ni dhahiri kuwa mama ndiye nayeumia zaidi pale familia inapokuwa na uchumi mbaya. Mama hapendi kuona watoto wanakosa mahitaji yao ya msingi kama vile chakula, mavazi, elimu, matibabu n.k.

Hivyo suala la kuboresha kipato cha familia limewafanya wanawake wengi kutafuta njia mbalimbali za kujipatia kipato ikiwemo njia ya kufanya biashara.

Hata hivyo pamoja na jitihada hizi zinazofanywa na wanawake, bado biashara zao ngingi hufa kutokana na sababu kadha wa kadha. Fuatana nami katika makala hii ufahamu mambo matano yanayosababisha biashara nyingi za wanawake kufa.

1. Kukosa maarifa na elimu ya biashara
Kitu chochote au kazi yoyote inahitaji maarifa stahiki ili uweze kuifanya kwa kwa ufanisi. Ni dhahiri kuwa wanawake wengi huanzisha biashara pasipo kujiandaa kimaarifa au kutafuta ujuzi unaohitajika katika kuendesha biashara husika. Kumbuka hapa sizungumzii elimu ya sekondari au chuo kikuu bali maarifa yatakayokuwezesha kuendesha biashara husika kwa ufanisi. Kwa mfano unahitaji kupata maarifa yatakayokuwezesha kufanya haya yafuatayo:

Utunzaji wa fedha (ikiwemo mikopo kama utakopa)
Utunzaji wa taarifa za biashara
Utafutaji wa wateja
Uandaaji na uboreshaji wa bidhaa, huduma n.k
Haya ni baadhi tu ya maarifa ya msingi ambayo mfanyabishara anatakiwa kuwa nayo. Mwanamke anayefanya biashara akijipatia maarifa haya ya kutosha hakika uendeshaji wa biashara yake utakuwa bora na wa uhakika; hivyo biashara yake itadumu zaidi. Maarifa haya yanaweza kupatikana bure katika taasisi zinazowawezesha wanawake pamoja na kwenye mtandao.

2. Kukosa msaada na ushirikiano
Ili kufanikiwa katika mambo kadha wa kadha tunahitaji ushirikiano ua msaada wa watu wengine kwa namna moja au nyingine. Simaanishi kuwa tuwategemee watu wengine kwa kila kitu; bali ukumbukue tu kuwa huwezi kufanya kila kitu peke yako. Wanawake wengi hukosa ushirikiano hasa katika ngazi ya familia.

Badala ya mume au wanafamilia wengine kumpa mwanamke huyu ushirikiano katika biashara yake wao huwa ni wa kwanza kumkejeli, kumkatisha tamaa, kumsema, kumlundikia mambo na hata kumwachia kila kitu peke yake. Matokeo yake mwanamke huyu huzidiwa na kushindwa kumudu biashara yake.

3. Kuiga au kukosa ubunifu
Wanawake wengi wanapoanzisha biashara hawatumii ubunifu bali wao hukurupuka kwa kuona biashara za wengine pekee. Kabla hujaanzisha biashara hakikisha unatumia ubunifu kubuni biashara yako.

Epuka kuiga kwani hujui ndani ya biashara unayoiga kuna nini; inawezekana kuna changamoto usizoziweza. Usione tu biashara kwa nje na kuirukia; hakikisha pia biashara unayoichagua unaipenda kutoka moyoni mwako.

4. Tamaa
Wanawake wengi huvutiwa na vitu mbalimbali hata kama hawavimudu kifedha. Leo umemwona rafiki yako ana simu au mkoba au hereni au viatu ama hata nguo fulani nawe unatamani kuwa nayo bila hata kujua gharama zake zikoje na utapataje pesa hizo. Hili limewapelekea wanawake wengi kutumia mitaji yao ya biashara kwa ajili ya tamaa na mashindano.

Mara kadhaa utasikia mwanamke anasema “nimekula mtaji”; kulikuwa na shunguli fulani au kitu fulani kilinigharimu. Hakika ukiendeleza taamaa hutoweza kuendesha biashara na ikafanikiwa. Ni lazima ujiwekee nidhamu katika matumizi yako ya fedha ili uweze kufanikiwa.

Mambo unayoweza Kufanya:

Tambua uwezo wa kipato chako ili ujiwekee mipaka.
Bainisha matumizi ya lazima.
Tenga pesa za biashara na maisha yako binafsi.
Weka akiba.
Epuka tamaa na vishawishi vya marafiki.


5. Majukumu ya kifamilia
Kiafrika mwanamke ndiye mwenye jukumu kubwa la kuwa karibu na familia yake. Si rahisi kwa mwanamke wa kiafrika kushinda kwenye biashara kwa siku nzima bila kuwa na utaratibu mwingine wa kutunza familia yake.

Swala hili limekuwa likiwafanya wanawake kutokuwa na muda mwingi wa kutulia na kushughulikia biashara zao; jambo hili limeathiri kwa kiasi kikubwa biashara nyingi za wanawake. Hata hivyo unaweza kufanya mambo yafuatayo ili kukabiliana na hili:



Tafuta usaidizi kwa baadhi ya majukumu yako ya biashara au ya nyumbani.
Tumia muda vyema (Punguza kazi zisizokuwa na ulazima – hakuna haja ya kukaa saluni siku nzima ukisuka wakati unaweza kupunguza nywele au kuzichana na kuzibana pekee.)
Shirikisha familia katika mgawanyo wa majukumu ili nao pia wakupunguzie kazi.
Chagua biashara ambayo unaipenda na unaimudu; hili litakupa ufanisi zaidi unapoifanyia kazi.

Hitimisho

Yaliyojadiliwa hapa ni baadhi ya mambo makubwa yanayosababisha biashara nyingi za wanawake kufa. Hata hivyo njia za kukabiliana na mambo haya zimejadiliwa pia; hivyo ni swala la wewe tu kufanya maamuzi ili uweze kumudu na kufanikiwa katika malengo yako ya kibiashara. Weka malengo leo na uyafuate ndipo utakapoweza kufanikiwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad