Mambo Safi..Ujerumani Yaipatia Tanzania Bilioni 190.5




Ujerumani imeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 71, sawa na takribani Sh190.5 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi kadhaa ikiwemo maji, uendelezaji wa maliasili na utalii, afya ya mama na mtoto pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Fedha na Mipango leo Jumanne Oktoba 26 2021 nyaraka za makubaliano ya msaada huo zimetiwa saini kati ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia masuala ya Fedha za Nje Amina Khamis Shaaban na Kiongozi wa ujumbe wa Serikali ya Ujerumani Marcus Von Essen.

Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa nyaraka hizo, Naibu Katibu Mkuu Amina Khamis Shaaban aliyataja maeneo yatakayonufaika na msaada huo kuwa ni afya ya mama na mtoto iliyotengewa Euro milioni 24 na mradi wa kuzuia migogoro baina ya wanyamapori na binadamu, utakao tumia Euro milioni 6.

“Maeneo mengine yatakayonufaika na fedha hizi ni mpango wa kufidia upotevu wa makusanyo ya maduhuli katika sekta ya utalii kutokana na upungufu wa watalii walioingia nchini kwa sababu ya ugonjwa wa Uviko -19,”amesema.


Ameyataja maeneo yatakayonufaika kuwa ni kuzuia ujangili, kuboresha miundombinu kwenye makazi na jamii inayozunguka maeneo ya Hifadhi za Taifa, utakaogharimu Euro milioni 15.

Alisema kuwa Euro milioni 20 zitaelekezwa kuboresha huduma ya maji kwenye miji inayokua na kiasi kingine cha Euro milioni 3 kitatumika kuboresha usalama wa maji kwenye maeneo ya baadhi ya miji nchini.

Amina amesema kuwa kiasi kingine cha Euro milioni 3 kitatumika katika masuala ya kulinda haki za akina mama na wasichana wanaokabiliwa na changamoto ya ukatili wa kijinsia kwa kuwapatia msaada wa kisheria.


Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess na Kiongozi wa Ujumbe wa Ujerumani ulioshiriki majadiliano yaliyofanikisha kupatikana kwa msaada huo Marcus Von Essen, walisema Ujerumani imeamua kufufua ushiriki wake katika kujenga maendeleo ya Tanzania ili kuunga mkono uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Walieleza kuwa chini ya makubaliano mapya, Ujerumani yatajikita zaidi kusaidia afya ya mama na mtoto, kusaidia masuala ya bima ya afya kupitia NHIF, maji na usafi wa mazingira, usimamizi wa fedha za umma, kuhifadhi maeneo ya urithi wa dunia kama vile hifadhi ya Selous na kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya vitendo vya kikatili.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad