Maafisa wa Marekani wamekutana na utawala wa Taliban wa Afghanistan kwa mazungumzo yao ya kwanza ya ana kwa ana tangu Washington ilipoondoa wanajeshi wake kutoka nchini humo mwezi Agosti.
Mazungumzo hayo nchini Qatar yanaangazia masuala ikiwa ni pamoja na kudhibiti vikundi vyenye msimamo mkali, uondoaji raia wa Marekani na misaada ya kibinadamu, maafisa wanasema.
Marekani inasisitiza mkutano huo hauna uhusiano na kutambuliwa kwa Taliban.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Afghanistan kupata shambulio baya kabisa tangu majeshi ya Marekani yalipojiondoa.
Shambulio la kujitoa muhanga katika msikiti mmoja katika mji wa kaskazini wa Kunduz liliwauwa watu wasiopungua 50 na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa.
Msikiti wa Said Abad ulitumiwa na jamii ndogo ya Waislamu wa Shia katika nchi iliyo na Waislamu wengi wa Kisunni. Kundi la Islamic State limesema lilitekeleza shambulio hilo.
Akiongea baada ya mazungumzo na Marekani kufunguliwa nchini Qatar, Waziri wa Mambo ya nje aliyeteuliwa na Taliban Amir Khan Muttaqi alisema pande hizo mbili zimekubali kuzingatia masharti ya makubaliano ya Doha yaliyosainiwa mnamo 2020.
Mkataba huo ni pamoja na majukumu makubwa kwa Taliban kuchukua hatua za kuzuia vikundi kama al-Qaeda vinavyotishia usalama wa Marekani na washirika wake.
Bwana Muttaqi alisema maafisa wa Marekani pia waliwaambia Taliban watasaidia katika kutoa chanjo za Covid na misaada ya kibinadamu.
Marekani bado haijasema chochote kuhusu mazungumzo ya Jumamosi, lakini msemaji wizara ya mambo ya nje hapo awali alisema maafisa watatumia mkutano huo kushinikiza Taliban kuheshimu haki za wanawake, kuunda serikali inayojumuisha na kuruhusu mashirika ya kibinadamu kufanya kazi.
Mkutano huo unaendelea siku ya Jumapili.
Bwana Muttaqi aliwaambia waandishi wa habari kuwa kundi la Kiisilamu linataka kuboresha uhusiano na jamii ya kimataifa lakini pia alionya kwamba hakuna mtu anayepaswa kuingilia sera za ndani za nchi hiyo.Bendera za Taliban zikiuzwa mjini Kabul
Maafisa wa Marekani wamesema mazungumzo hayo ni mwendelezo wa kushirikiana na Taliban kuhusu mambo ya masilahi ya kitaifa, sio kuhusu kutoa uhalali kwa serikali ya kikundi hicho.