Shule tatu za msingi katika jimbo la New York zimepiga marufuku mavazi ya Halloween yanayofanana na yale yaliyovaliwa na washiriki wa kipindi cha tamthilia maarufu ya Netflix, Squid Game, kwa kuhofia kwamba yanaweza kuchochea vurugu. Tamthilia hiyo ya kusisimua ya Korea Kusini inaeleza kuhusu hadithi ya watu wazima wanaoshindania zawadi ya pesa kwa kucheza michezo ya watoto, na ambao wako tayari kuhatarisha maisha yao ili kushinda.
Maudhui yake yanayoonekana kwenda kinyume na maadili kwa baadhi ya jamii yamesababisha shule kuwatumia barua pepe wazazi kuhusu “ujumbe wa uchochezi” wa tamthilia hiyo.
Shule hizo zimesema mavazi ya Mchezo wa Squid katika hafla za shule “hayatafaa”.
Miongozo ya Shule ya Fayetteville-Manlius ya New York inapiga marufuku mavazi ya Halloween yenye vitu “vinavyoweza kufasiriwa kama silaha”, na vile “vya kuchukiza sana au vya kutisha”, Msimamizi wake Dokta Craig Tice aliiambia CBS News.
Nchini Marekani, tamthilia hiyo imewekwa na mtandao wa Netflix kwenye darala la kuangaliwa na hadhira ya watu wazima, kumaanisha kwamba kipindi hicho cha Televisheni “huenda kisifae kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 17”.
Lakini baadhi ya wazazi wanaripotiwa kutofurahishwa na marufuku hiyo ya mavazi iliyotolewa na shule hizo. “Ni vazi tu. Cha kufanya usiruhusu watoto wako kutazama kipindi,” mwanamke mmoja aliiambia CBS.