KAMISHNA Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhan Kingai, amedai Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alitoa maelekezo ya kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, kwa kumpulizia poda ya sumu usoni.
Amedai kuwa kiongozi huyo wa CHADEMA alitoa maelekezo hayo kwa madai Sabaya ni kikwazo kwake kulipata Jimbo la Hai.
Hata hivyo, kutokana na madai hayo, upande wa utetezi umeibua hoja saba ulizozielekeza kwa shahidi huyo, ukitaka ufafanuzi.
Kingai alidai hayo jana alipotoa ushahidi Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Joackim Tiganga kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando.
Alidai katika maelezo ya onyo aliyotoa mshtakiwa wa pili, Adamu Kasekwa, maarufu Adamo, Julai 24, 2020, akiwa na mshtakiwa wa tatu, Mohammed Ling'wenya, walikutana na Luteni Dennis Urio Morogoro, na aliwafahamisha kuna kazi ya ulinzi wa kiongozi kwa Mbowe.
Shahidi huyo anadai Urio aliwapa Sh. 87,000 kila mmoja kwa ajili ya kwenda Moshi na walifika Moshi saa 10 alfajiri wakapokewa na dereva wa Mbowe aliyeitwa Willy akiwa na Pickup ya Chadema M4C, wakapelekwa Hoteli ya Aishi kulala.
Katika maelezo hayo, Kasekwa alidai asubuhi walitambulishwa kwa Mbowe na mshtakiwa Halfani Bwire na ilipofika saa tano usiku, walifanya kikao wakiwa watu watano.
"Tulifanya kikao na Mbowe Julai 24, mwaka 2020, tukiwa watano, Mbowe, Ling'wenya, Moses Lijenje na Bwire, alitupa maelekezo. Alisema Sabaya anamvuruga sana, anawavuruga wapigakura wake wa Jimbo la Hai, amesababisha fedha za ruzuku za CHADEMA zimeshushwa.
"Anayofanya Sabaya yanamtia wasiwasi, yanahatarisha kuukosa ubunge, tuweke miundombinu ya kumdhuru ili asifanikiwe kufanya mambo yake ili Mbowe apite.
"Alituelekeza kumdhuru kwa namna yoyote ile, tulipanga kumdhuru kwa kumpulizia poda ya sumu usoni. Julai 26, 2020, tulirudi Dar es Salaam.
"Tulipofika tulipewa Sh. 200,000 kwa ajili ya maandalizi ya mavazi ya kumpokea Tundu Lissu Uwanja wa Ndege. Julai 31, 2020 tulirudi Moshi na tulipewa nauli Sh. 78,000.
"Tulipofika Moshi tulimkuta Mbowe na Bwire wako Aishi Hoteli. Alfajiri ya Agosti Mosi, 2020, Mbowe wakati anataka kurudi Dar es Salaam, alituita alituelekeza azma yake ya kumdhuru Sabaya, alituonyesha picha ya Sabaya kupitia simu yake ya kiganjani, alituambia anapatikana katika Klabu ya Kokoliko.
"Mbowe alituacha Moshi, tulianza kumtafuta Sabaya Boma Ng'ombe, Kokoliko na Way Stone hatukumwona, kazi hiyo tulifanya Agosti 3 na 4 mwaka 2020 na Agosti 5 tuliamua kwenda Rau Madukani kwa dada yake Ling'wenya ili kubana matumizi kwa sababu tuliachiwa kiasi kidogo, Sh. 150,000 isingetosha kujikimu.
"Alituambia baada ya kumaliza kazi hiyo atatupa kazi nyingine ya kulipua vituo vya mafuta, kukata miti barabarani, kuratibu maandamano yasiyo na kikomo ili kuonyesha serikali imefeli kuelekea Uchaguzi Mkuu," alidai hayo yalikuwa maelezo ya Kasekwa.
ACP Kingai alidai kuwa Kasekwa alikiri kukamatwa na polisi Agosti 5, 2020 wakiwa Rau Madukani, alikiri kukutwa na pisto yenye risasi tatu, alikiri kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroine kete 58.
Anadai walimtafuta mshtakiwa Bwire na kufanikiwa kumkamata, walipofanya upekuzi nyumbani kwake maeneo ya Temeke, walimkuta akiwa na sare za JWTZ pamoja na vifaa vingine vya jeshi na vitendo vya kigaidi walipanga kufanya Moshi, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza.
HOJA SABA ZA UTETEZI
Hata hivyo, upande wa utetezi uliibua hoja saba wakati ukimhoji shahidi hiyo, ikiwa ni pamoja na washtakiwa kukamatwa wakiwa hawana vifaa vyovyote vya ulipuaji, ukataji miti na kuchukuliwa alama za vidole ili kujiridhisha kama walishika silaha husika.
Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Jeremiah Mtobesya, ACP Kingai alidai ushiriki wa Luteni Dennis Urio ulikuwa ni kuwatafuta vijana wa kufanya kazi kwa Mbowe na kuwapa fedha zilizotoka kwa Mbowe.
Akihojiwa na Wakili John Mallya, ACP Kingai alidai alichukua maelezo ya onyo kupitia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 57 na 58 sura ya 20 ya mwaka 2018, lakini imekosewa na wachapaji ilipaswa kuwa mwaka 2002 na si 2018.
Akihojiwa na Wakili Peter Kibatala, ACP Kingai alidai hawajawakamata washtakiwa wakiwa na kifaa chochote cha ulipuaji wa vituo vya mafuta, kukata miti wala kipeperushi cha kufanya maandamano mikoa ya Dar es Salaam, Moshi, Arusha, Morogoro na Mwanza.
Alidai katika ushahidi wake hakuzungumzia lolote kuhusu washtakiwa wote kukutana Arusha na hafahamu kama washtakiwa waliwahi kufanya kikao Morogoro.
ACP Kingai alidai alitoa onyo kwa kosa la kufanya ugaidi, lakini hakumwonya Kasekwa kwa kufanya kikao na hakumwonya kwa shtaka la nne la kukutwa na pisto na aliongeza kuwa hajawahi kuchukua alama za vidole kujiridhisha kwamba Kasekwa aliishika silaha hiyo.
Pia shahidi huyo wa kwanza alidai walichukua simu za watoto wa Mbowe na baada ya uchunguzi, walibaini hazihusiani na kesi hiyo lakini simu hizo hazijarudishwa na alipokea maombi ya kuzitaka wiki mbili au tatu zilizopita.
Alidai hakuwahi kumfahamisha Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kesi hiyo na upelelezi wake wala hakuwahi kutoa taarifa kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhusu tukio la kumdhuru Sabaya.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Bwire, Kasekwa, Ling'wenya na Mbowe ambao wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya kula njama kufanya vitendo vya kigaidi, ikiwamo kulipua vituo vya mafuta na kumdhuru Sabaya. Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea leo.