WINGA mpya wa Yanga, Jesus Ducapel Moloko, amesema kuwa tangu atue klabuni hapo, amebaini kuwa klabu hiyo ina mashabiki wengi zaidi ya AS Vita ya nchini DR Congo.
Moloko amejiunga na Yanga katika dirisha kubwa la usajili lililopita ambapo alisajiliwa kuwa mbadala wa winga Tuisila Kisinda ambaye alitimkia RS Berkane ya nchini Morocco.
Winga huyo tangu ajiunge na Yanga, amekuwa sehemu ya kikosi cha kwanza ambapo tayari amefanikiwa kuifungia timu hiyo bao moja katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Geita Gold ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Moloko alisema kuwa tangu ajiunge na klabu hiyo, amebaini kuwa klabu hiyo ina mashabiki wengi kuliko klabu yake ya awali ya AS Vita ambayo alikuwa akicheza soka kabla ya kuhamia Yanga.
“Yanga ina mashabiki wengi kuizidi AS Vita, hilo nimeliona angu nimetua ndani ya Yanga, namba ya watu wanaonifuatilia kupitia mitandao ya kijamii ni kubwa sana lakini hata mapokezi ambayo tumekuwa tukiyapata mikoani na hata mashabiki ambao wanahudhuria katika mechi za Yanga ni wengi zaidi ya AS Vita ambapo mashabiki ni wachache wanaohudhuria katika mechi,” alisema winga huyo.
“Mtandaoni ndipo kunaposhangaza kwani nimepata watu wengi sana wanaonifuatilia kupitia Yanga, wakati nikiwa AS Vita wala sikuwa na watu wengi wanaonifuatilia licha ya kucheza katika sehemu kubwa ya timu, baada ya kutua Yanga kila kitu kilibadilika na nilishangaa sana ukubwa nilioupata.”