Polisi nchini Norway imesema mtu aliyewauwa watu watano kwa upinde na mishale na silaha nyingine huenda alikuwa na matatizo ya kiakili.
Inspekta wa Polisi Per Thomas Omholt ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kuwa maafisa walichunguza masuala kadhaa, ikiwemo hasira, kulipiza kisasi, itikadi kali, magonjwa, uchokozi, na kukubaliana kuwa hoja inayoonekana kuwa ya msingi katika siku hizi za kwanza za uchunguzi ni kuwa historia yake ni ya maradhi.
Mshukiwa huyo raia wa Denmark mwenye umri wa miaka 37, Espen Andersen Braathen, amekiri kuwauwa watu hao watano na anaendelea kushirikiana katika uchunguzi.
Mapema leo, mahakama iliamuru kuwa Braathen aendelee kushikiliwa kizuizini kwa hadi wiki nne kabla ya kusikilizwa kesi yake.