Abdulrazak Gurnah huwenda likawa ni jina jipya kabisa masikioni mwako ila huyu ni Mtanzania aliyezaliwa Zanzibar mwaka 1948 ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Kent, Uingereza na mtunzi maarufu wa vitabu ambaye amefanikiwa kushinda tuzo ya Nobel ya Fasihi 2021 huko Stockholm nchini Sweden.
Tuzo hiyo inamfanya kuwa Mwafrika wa pili kushinda na imetangazwa mapema wiki hii na Mats Malm ambaye ni katibu wa kudumu wa Swedish Academy na katika uandishi wake unatajwa kuchochea mabadiliko makubwa kwenye Jamii ikiwemo kuelezea athari za ukoloni na hatima ya wakimbizi.
Gurnah ameandika riwaya takribani 10 kama ‘Memory of Departure’, ‘The Last Gift’, ‘Paradise’ na kadhalika. Gurnah ametangazwa Alhamis Oktoba 7 na Chuo cha Sweden kuwa mshindi wa taji hilo lenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.14 sawa na Sh bilioni 2.627.
“Kujitoa kwa Abdulrazak Gurnah kuhusu ukweli na kuchukia kwake kurahisisha mambo kunashangaza,” Kamati ya Nobel ya Fasihi imesema katika taarifa yake.
“Riwaya zake zinaelezea ubaguzi na kubainisha mawanda mapana ya tamaduni za nchi za Afrika Mashariki ambazo hazikufahamika kwa wengi ulimwenguni kote.”