KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amewataka mashabiki wa timu hiyo kutulia na si kuanza kukosoa kiwango cha kikosi hicho kwani watarejea wakiwa bora zaidi baada ya ligi kusimama.
Nabi ametoa kauli hiyo baada ya Yanga kushinda mechi mbili za kwanza za ligi na moja ya Ngao ya Jamii kwa matokeo ya 1-0 ikizifunga Simba, Kagera Sugar na Geita Gold.
Akizungumza na Spoti Xtra, Nabi alisema: “Kitu cha kwanza ambacho kwetu ni bora ni kuwa bado tumepata matokeo mazuri katika mechi tatu, kuanzia ile ya Simba na mbili za ligi ingawa bado tumekuwa na shida katika kipindi cha pili kwa kukosa muunganiko na nguvu za kushambulia.
“Lakini matumaini yetu hili jambo litafikia kikomo kwa kuwa tunaenda Arusha kwa ajili ya kambi maalum katika kipindi hiki kifupi cha mapumziko, tunaamini tutarejea tukiwa kwenye ubora mkubwa.
“Tunajua ligi ni ngumu na imekuwa na ushindani mkubwa, lakini tunataka kuona ukubwa na nguvu ambayo tunaanza nayo ndiyo tutamaliza nayo, hivyo mashabiki wanapaswa kutulia.