KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ametamba kuwa baada ya kupata ushindi kwenye michezo yao miwili ya kwanza ya Ligi Kuu Bara moto wao hautazimwa kwani watahakikisha wanashinda mechi zote zinazokuja.
Nabi tayari ameiongoza Yanga katika michezo miwili ya ushindi kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold, ushindi ambao unaifanya Yanga kukamatia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa kujikusanyia pointi sita.
Licha ya matokeo hayo Nabi amekiri sehemu kubwa ya kikosi chake inakosa utimamu wa mwili, jambo ambalo wamepanga kulifanyia kazi wakati huu ligi ikiwa imesimama kuptisha mechi za kimataifa zilizo kwenye kalenda ya Fifa.
Akizungumza na Championi Jumatano, Nabi alisema: “Tunafurahia kuanza ligi kwa matokeo ya ushindi katika michezo yetu miwili ya kwanza, ni jambo la muhimu kushinda pointi tatu kwenye kila mchezo lakini bado tuna changamoto kadhaa za kiufundi kama vile utimamu wa mwili wa wachezaji, hali ambayo imechangiwa na changamoto kwenye maandalizi ya msimu ‘Pre season’.
“Hivyo kama benchi la ufundi tumejipanga kuwekeza kwenye mazoezi ya utimamu wa mwili ambayo yatawafanya wachezaji wetu wake na uwezo wa kustahimili mchezo kwa dakika nyingi.”
Musa Mateja na Leen Essau, Dar es Salaam