MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti amesikitishwa na kitendo cha Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kutokamilisha uwekaji madawati katika Shule ya Msingi Ntanganyika iliyopo Kijiji cha Chala Wilaya ya Nkasi.
Hayo yamejiri jana Ijumaa, Oktoba 22, 2021 wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipokutana na wananchi wa kijiji cha Chala na kuzungumza nao ambapo kwa kauli moja wamekubaliana kuanzia sasa hatua za kuchangia ili madawati yapatikane.
“Sijafurahishwa kuona sasa ni mara ya tatu nafika kwenye shule hii na kukuta karibu ya asilimia 60 ya wanafunzi wanakaa chini bila madawati. Hii si sawa, sihitaji tena kuona watoto kukaa chini wakati Wilaya ya Nkasi ina misitu ya kutosha na sisi viongozi tupo,” alisema Mkirikiti.
Kwa upande wake Diana Mndeme ambaye ni Afisa Tarafa wa Chala amesema si katika shule ya Ntanganyika pekee kwenye upungufu wa madawati hivyo atapita kwenye kata zote na kuhamasisha wazazi kuchangia upatikanaji wa madawati.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijuakali amesema tatizo la ukosefu wa madawati limechangiwa na usimamizi mbovu wa watendaji wa kata na vijiji hivyo atafuatilia kwa karibu.