Asilimia kubwa ya maradhi yanayowasumbua watu hivi leo yanatokana na sumu zilizopo katika miili yao. Inawezekana umewahi kusikia mambo mengi kuhusu sumu kwenye mwili, lakini hufahamu chazo halisi cha sumu hizi.
Mabadiliko ya mazingira na mtindo wa maisha hupelekea kutengenezeka na kuingia kwa sumu nyingi ndani ya mwili wa binadamu. Sumu hizi hutokana na vyakula, vinywaji na hata mazingira tunayoishi.
Sumu hizi huweza kuleta madhara makubwa mwilini kama vile kushindwa kufanya kazi kwa viungo vya mwili na hata aina mbalimbali za saratani.
Ni vyema ukafahamu njia bora za kuondoa sumu mwilini mwako ambazo unaweza kuzifanya wewe mwenyewe bila gharama za ziada.
Kula vyakula vya asili
Hivi leo watu hufikiri kula vyakula vya asili ni kupitwa na wakati. Wengi husifu vyakula vya viwandani na vile vya kukaangwa kuwa ndivyo vyakula bora. Vyakula kama vile Chipsi, nyama, Baga, na tambi ni baadhi tu ya vyakula ambavyo vinaonekana kuwa vya kisasa na bora zaidi, lakini katika uhalisia manufaa yake mwilini ni kidogo.
Ili uweze kuondoa sumu mwilini mwako ni vyema ukaepuka vyakula hivi kwani huwa vina viini vinavyojenga sumu mwili. Jizoeze kula vyakula vya kuchemsha zaidi tena vya asili. Matunda na mbogamboga zisizo na madawa zitakufaa zaidi.
Kunywa maji mengi
Ni dhahiri kuwa miili yetu imejengwa kwa maji asilimia 70, hivyo kunywa vinywaji kama vile soda na sharubati (juice) za viwandani kunaongeza sumu mwilini.
Ni muhimu kufahamu kuwa ufanyaji kazi wa viungo kama vile figo hutegemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa maji ya kutosha mwilini. Hivyo maji yakikosekana ni dhahiri kuwa sumu nyingi sana hazitaondolea mwilini kwa njia ya msingi ya haja ndogo.
Fanya mazoezi
Watu wengi hasa Waafrika hawana utaratibu wa kufanya mazoezi. Kufanya mazoezi kutakuwezesha viungo vyako vya mwili kufanya kazi ipasavyo. Ni dhahiri pia unapofanya mazoezi utatokwa na jasho; na hii ni njia nzuri ya kutoa taka mwilini ikiwemo sumu zilizoingia katika mwili wako. Unaweza kufanya mazoezi ndani au hata nje kutegemea vile unavyopendelea.
Punguza mafuta
Inawezekana unapenda kula vyakula vyenye mafuta mengi; hili si jambo zuri kwa ajili ya afya yako. Jizoeze kupunguza ama kuepuka mafuta katika vyakula vile unavyokula kwani si aina zote za mafuta zinafaa kwenye mwili wako.
Jitahidi kuepuka na kupunguza ulaji wa mafuta kadri uwezavyo ili uweze kuondoa sumu mwilini mwako.
Kula vyakula vya nyuzinyuzi
Unatakiwa kufahamu kuwa vyakula vyenye nyuzinyuzi ni vizuri pia katika kusafisha mwili na kuondoa sumu au takataka mbalimbali.
Vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi ni pamoja na parachichi, ndizi, peazi, karoti, pilipili hoho, mchele wa brown (wanaoutumia watu wa kisukari), maharage meusi, njegere, tende, viazi vitamu, tofaa (apple), machungwa, ugali wa dona pia mkate wa unga wa ngano ambao haujakobolewa. Ulaji wa vyakula hivi utakuwezesha kuondoa kiasi kikubwa cha sumu mwilini.
Epuka matumizi ya pombe
Kama ilivyo kwa vyakula vya viwandani, pombe nyingi hutengenezwa kwa kutumia kemikali mbalimbali ambazo nyingine ni hatari kwa afya yako. Ili kuondoa na kupunguza kiasi cha sumu zinazoingia mwilini mwako jitahidi kuepuka matumizi ya pombe na kutumia vinywaji vingine kama vile maji.
Ni dhahiri kuwa sumu nyingi huingia katika miili yetu kutokana na mtindo wa maisha au mazingira yetu yasiyozingatia kanuni za msingi za afya bora. Mwili wa binadamu uliumbwa kutegemea na kutumia vitu halisi na si visivyo halisi (artificial).
Hivyo jitahidi kuwa mtu mwenye kupenda mboga na matunda zaidi kuliko vyakula vingine, ili uweze kupunguza kiasi cha sumu kinachoingia kweye mwili wako.