Kijana huyu mwenye umri wa miaka 23 Sandile Shezi ambaye anajiita 'milionea mwenye umri mdogo zaidi' nchini Afrika Kusini alikamatwa na maafisa wa polisi.
Afisa wa polisi wa eneo la Gauteng nchini Afrika Kusini Mavela Masondo anasema kwamba Shezi alijiwasilisha mwenyewe katika kituo cha polisi akiandamana na wakili wake.
Polisi walimfungulia mashtaka ya ulaghai kijana huyo ambayo alikana.
'Naweza kuthibitisha kwamba polisi walimkamata kijana huyo. Aliwasilishwa mbele ya hakimu wa eneo la Randburg siku ya Alhamisi ambapo alishtakiwa na mashtaka ya ulaghai', alisema bwana Masondo.
Shezi ambaye alikuwa ametoka katika mji wa Durban anadaiwa kumlaghai mfanyabishara mwenza wa kampuni ya Global Forex Institute GFI kima cha R500,000 ambazo ni sawa na $34,264.
Maafisa wa polisi walikuwa wametoa kibali cha kumkamata mapema mwezi huu .
Sandile Innocent Shezi amekuwa akijiita milionea mwenye umri mdogo zaidi , pamoja na mwenzake walianzisha biashara ya fedha za kigeni.
GFI ni kampuni inayowafunza watu kuhusu biashara ya fedha za kigeni ambapo huwafunza watu kuanzisha biashara zao.
Alianza ndoto yake ya kufanya biashara akiwa na umri mdogo ambapo alikuwa akichukua fedha kutoka kwa rafiki zake ili kufanya biashara.