Rais Apewa Siku 14 na Mahakama Kuapisha Majaji 6 Lasivyo....




MVUTANO kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Idara ya Mahakama kuhusu uteuzi wa majaji sita wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu ulichukua mkondo mpya Alhamisi, baada ya kiongozi wa nchi kuagizwa kuwaapisha katika muda wa siku 14.

Iwapo Rais Kenyatta atafeli kuwaapisha ndani ya muda huo, Mahakama Kuu iliagiza Jaji Mkuu Martha Koome na Tume ya Huduma kwa Mahakama (JSC) kuwaapisha na waanze majukumu yao mapya mara moja.

“Baada ya siku 14 kukamilika na Rais Kenyatta hatakuwa amewaapisha majaji hawa sita, basi Jaji Koome na JSC wachukue hatua ifaayo ya kuwaapisha majaji hao ili waanze kutekeleza kazi zao mara moja,” waliagiza Majaji George Dulu, William Musyoka na James Wakiaga.

Majaji hao walisema tangu 2019 Rais Kenyatta hakuwaapisha baada ya kuteuliwa na JSC kwa mujibu wa sheria.Majaji hao sita ambao Rais Kenyatta alikataa kuwaapisha ni George Odunga, Aggrey Muchelule, Joel Ngugi na Weldon Korir, walioteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa.


Wengine ni Bw Evans Makori na naibu wa msajili wa mahakama kuu, Bi Judith Omange.

Bw Makori na Bi Omange waliteuliwa na JSC kuwa majaji kitengo cha Masuala ya Ardhi na Mazingira.

Jaji Ngugi na Jaji Odunga walikuwa miongoni mwa majaji watano waliotupilia mbali Mswada wa Marekebisho ya Katiba (BBI).


“Rais Kenyatta ameshindwa kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ya kuwaapisha majaji hao sita aliochelea kuwateua na kuwaapisha tangu 2019,” wakasema majaji hao.

Majaji Dulu, Musyoka na Wakiaga walisema imebidi mahakama itoe maagizo hayo kwa vile Katiba haijatoa mwelekeo wa hatua itakayochukuliwa dhidi ya Rais “akikaidi na kukataa kutekeleza majukumu aliyopewa na Katiba.”


Majaji George Dulu, William Musyoka na James Wakiaga (kushoto) katika Mahakama Kuu ya Nairobi, Oktoba 21, 2021. Picha/ Dennis Onsongo
Majaji hao walisema siku 14 zikipita bila ya Rais Kenyatta kuwaapisha majaji hao sita basi “itaeleweka hana mamlaka tena kutenda majukumu yake.”

Majaji hawa sita walikuwa miongoni mwa majaji 41 walioteuliwa 2019 kisha Rais Kenyatta akachelea kuwateua akidai baadhi yao walihusika na ufisadi.


Majaji Dulu, Musyoka na Wakiaga walisema kuzembea kwa Rais Kenyatta kutekeleza majukumu yake kumewafanya watoe maagizo hayo.

Kesi hii ya kuwapa mamlaka Jaji Mkuu na JSC kuwaapisha majaji hao iliwasilishwa na walalamishi kadhaa miongoni mwao wakili Adrian Kamotho.

Kama adhabu, majaji hao waliamuru afisi ya Rais ilipe gharama ya kesi hiyo.Majaji hao walitupilia mbali ombi la Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki wasitishe kesi hiyo ya majaji hao sita kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.

Bw Kihara alikata rufaa kupinga uamuzi wa majaji watano waliomwamuru Rais Kenyatta awaapishe majaji hao.


Baada ya kuteuliwa na kuapishwa kwa Jaji Martha Koome kuwa Jaji Mkuu wa tatu kuchukua nafasi ya Jaji Mkuu aliyestaafu David Maraga, Rais Kenyatta aliwaapisha majaji 34 na kuwaacha hao sita.

Kupitia kwa wakili Danstan Omari, majaji hao walishtaki serikali wakidai walikuwa wamebaguliwa.

Jana Alhamisi walipata afueni mahakama ilipoamuru rais awaapishe.

Na wakati huo huo Bw Kihara aliponea kutangazwa kuwa hafai kuhudumu katika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu kutokana na ushauri anaotoa kwa Serikali na haswa Rais kuhusu suala la uteuzi wa majaji 41.

Walalamishi kuhusu uteuzi huu wa majaji sita waliomba mahakama imtimue kazini Bw Kariuki kwa kutoa ushauri usiofaa kwa rais.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad