Rais Dk. Mwinyi atoboa siri ndege za ATCL kupokewa Zanzibar




RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Visiwani humo, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema uamuzi wa mapokezi ya ndege mbili mpya za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kufanyika Zanzibar, ni kielelezo cha juhudi za viongozi katika kuulinda na kuudumisha muungano. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea). 

Rais Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Oktoba, 2021 Visiwani Zanzibar wakati akipokea ndege hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Amesema katika ndege zote zilizonunuliwa, zilipokewa jijini Dar es salaam na Mwanza lakini uamuzi wa sasa ni wa kihistoria kwani umelenga kuendeleza juhudi za viongozi wa Taifa katika kuendelea kuulinda fikra, mawazo na falsafa za waaasisi wake.

Amesema ATCL ambayo ilianzishwa mwaka 1977, sasa inamiliki ndege 11 kati ya hizo ni Bombardier Dash 8 Q4100, Bombardier CS300, Boeing 787 dream liner lakini lengo ni kuwezesha shirika hilo kuwa na ndege 16 ifikapo mwaka 2023.


 

“Haya ni mafanikio makubwa tukizingatia kwamba sekta ya usafiri wa anga, majini na nchi kavu ni msingi muhimu wa maendeleo ya Taifa letu.

“Serikali zote mbili zimeahidi kuimarisha miundombinu kuwa ya kisasa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuboresha kiwanja cha ndege Pemba ili kuwa kisasa,” amesema.

Pia ameuagiza uongozi wa ATCL kuendelea kubuni na kuongeza mikakati imara ya kutumia changamoto zilizotokana na janga la maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 kuwa fursa.


“Pia ili kuhimili ushindani mkubwa wa sekta ya usafiri wa anga, Shirika lifuate miongozo ya usalama na afya ya kimataifa.

“Licha ya idadi ya watanzania kukadiriwa kufikia milioni 60, bado idadi ndogo ya Watanzania wanatumia usafiri wa anga, ni kazi ya ATCL kuwashajihisha watumie usafiri wa ndege kwani kadiri tutakavyotumia bei itashuka na shirika kupata faida,” amesema.

Pamoja na mambo mengine amesema Serikali Zanzibar itaendelea kuibua masoko mapya ya utalii hasa mashariki ya kati na mbali kwani kukiwepo na ndege za safari za moja kwa moja, zitaimarisha sekta hizo.

Pia amesema Serikali Mapinduzi Zanzibar imepokea ombi lililotolewa na ATCL kuhusu uhitaji wa jengo la kupumzikia wateja wao kwenye uwanja cha ndege Amani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad