Watu 100 wauwawa katika shambulio la bomu Afghanistan
Muungwana Blog 2 Oct 8, 2021
Mashambulizi katika msikiti mmoja wa kaskazini mwa Afghanistan, yaliyowalenga waumini wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia, yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 100 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.
Bomu liliripuka katika msikiti wa Gozar-e-Sayed Abad wakati wa sala ya Ijumaa. Ali Reza mmoja ya walioshuhudia tukio hilo amesema alikuwa anaswali wakati wa mripuko na ameripoti kuona majeruhi wengi.
Picha na vidio za matukio zimeonyesha waokoaji wakibeba miili iliyokuwa imefungwa ndani ya blanketi kutoka msikitini hadi katika gari la kubebea wagonjwa.
Ngazi za kuingilia msikiti huo zote zilikuwa zimejaa damu.
Naibu polisi wa mkoa wa Kunduz, Dost Mohammad Obaida, amesema hakuna kundi lolote hadi sasa lililokiri kuhusika na shambulio hilo lakini wanamgambo wa kundi la dola la Kiislamu wana historia ya muda mrefu ya kuwashambulia waumini walio wachache wa Shia.