Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta asema Afrika iko njia panda





Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema Afrika iko njia panda kutokana na changamoto inazozikabili, moja ikiwa ni mageuzi ya kiuchumi na pili ni mapambano juu ya ugaidi unaoongezeka na uasi katika bara hilo lenye mataifa 54
Akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo Kenya linashikilia urais wake kwa mwezi huu, Kenyatta amesema maandamano ya kutaka mageuzi ya mwaka 2011 yaliyoungwa mkono na Jumuiya ya Kujihami NATO kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu wa Libya, Moammar Gaddafi, yaliigawa nchi hiyo katika makundi mawili hasimu, kuibuka kwa kundi la Al Qaeda na kundi la wanamgambo wanaojiita Dola la Kiislamu, na kuzuka kwa makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na mataifa ya kigeni, ni mambo yanayotoa changamoto kubwa ya kijamii na kiuchumi barani Afrika.

Kenyatta amesema changamoto hizi zimechochewa zaidi na ongezeko la mapinduzi barani humo na janga la corona lililorejesha nyuma uchumi na kuyaweka mataifa mengi ya kiafrika katika umasikini, jambo ambalo walikuwa wameshaliepuka kutokana ukuaji wa uchumi ndani ya miongo miwili iliyopita.

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo, amegusia masuala kadhaa yanayotishia uhuru wa baadhi ya mataifa ya Afrika na ukosefu wa uthabiti unaochangiwa na masilahi ya pande tofauti sio tu katika maeneo yalio na mgogoro lakini hata nje ya bara hilo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amegusia mambo yanayotia wasiwasi barani humo, jeshi kuchukua madaraka katika mataifa mengi ya Afrika, janga la COVID 19 lililozidisha umasikini, ukosefu wa usawa wa kijinsia na chanzo cha migogoro mengi.

Kando na mambo ya kukatisha tamaa yaliyozungumziwa katika mkutano huo, Antonio Guterres amesema kuna mambo mengine mazuri ya kuigwa barani humo akitolea mfano wa uchaguzi wa amani uliofanyika Burkina Faso na hatua ya kukabidhiana madaraka iliyofanyika kwa amani nchini Niger na Zambia kufuatia uchaguzi wa rais.

Katika taarifa yake iliyosomwa na Naibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, Guterres amewapongeza watu wa Afrika akisema wanajitahidi kufanya kazi bila kuchoka kwa mustakabali mzuri wa bara lao pamoja na amani.

Kenyatta na Akuffo Addo kwa pamoja wamesema Umoja wa Afrika umechukua hatua hatua zinazonuiwa kuepusha migogoro, kukukuza amani na kujaribu kupambana na kutokomeza makundi yaliyo na itikadi kali. Kenyatta ametaka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya za kikanda kuisadia Afrika kuondokana na kitisho cha usalama katika eneo la Sahel, pembe ya Afrika, Afrika ya kati na katika mataifa yanayokumbana na uasi na makundi hatari ya kigaidi.

Hotuba za viongozi waliozungumza katika mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana juu ya ushirikiano kati ya Umoja huo na Umoja wa Afrika zilionyesha changamoto na migogoro inayoikumba bara hilo ambako chini ya asilimia 5 ya watu wake wamechomwa chanjo ya COVID 19. Athari za mabadiliko ya tabia nchi pia zinachangia kushuka kwa uchumi na kuongezeka kwa migogoro ya rasilimali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad