Rais wa Rwanda Paul Kagame amemsamehe waziri mkuu wa zamani Pierre Damien Habumuremyi ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kughushi hundi .
“Kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa”, ilisoma taarifa kutoka mkutano wa mawaziri wa kufikia azimio hilo ambao ulifanyika Jumatano, Rais Kagame alitoa msamaha kwa bwana Pierre Damien Habumuremyi.”
Mtoto wake Appollo Mucyo, ambaye alikuwa na kampeni katika mitandao ya kijamii ya kutaka baba yake aachiwe huru aliandika kwenye Instagram: “Moyo wangu umejawa na furaha isiyo na kifani , sina maneno sahihi ya kueleza jinsi nilivyofurahi.
“Ninamshukuru Mungu kwa yote, upendo nilionao kwa nchi yangu …bado uko vilevile.Ninashukuru…”
Bwana Habumuremyi,mwenye umri wa miaka 60, alikuwa waziri mkuu wa tisa kuanzia mwaka 2011 mpaka 2014,kabla ya hapo alikuwa waziri wa elimu.
Mwaka jana mwezi Novemba, alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kughushi hundi ambayo aliitoa katika chuo kikuu cha Kigali- Christian University of Rwanda, ambacho tangu wakati huo kilikuwa kimefungwa.
Alitakiwa kulipa $879,811 kama fidia.
Chombo cha habari cha taifa kiliripoti Alhamisi kuwa bado anahitajika kulipa fedha hizo na akifanikiwa hilo ndio akaunti zake za benki zitafunguliwa na kuachiwa mali zake zilizotaifishwa.
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo bwana Habumuremyi alisema alitoa hundi kama dhamana kwasababu wapokeaji wote walikuwa wamepokea fedha zao.
Mpaka alipokamatwa Julai 2020, alikuwa kiongozi wa kansela ya mashujaa , amri za taifa na mapambo ya heshima.