RC Awatolea Uvivu askari Barabarani Wala Rushwa



MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, amewashukia baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo ambao wamekuwa wakiendelea kuendekeza vitendo vya rushwa, kwa kupokea pesa za madereva wanaokiuka kwa makusudi sheria barabarani.

Mongela, alisema kuna askari wanaochafua taswira ya Jeshi la Polisi hivi sasa, kutokana na kufumbia macho magari mabovu pamoja mabasi yanayokwenda mwendo kasi na kuhatarisha usalama wa abiria.

Mongela alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wakazi wa mkoa huo, baada ya kuzindua rasmi kampeni ya ukaguzi wa vyombo vya moto kuelekea maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.

Maadhimisho hayo kitaifa mwaka huu yatafanyika mkoani Arusha, kuanzia Novemba 15 hadi Novemba 20.

“Ninawaonya tu hao askari na hata madereva na makondakta mnaoshiriki vitendo vya rushwa, acheni mara moja. Rushwa ni adui wa haki na kufanya hivyo ni kukosa uadilifu,"alisema Mongela.


Mongela pia alilipongeza Jeshi la Polisi, kwa kupunguza matukio ya ajali za barabarani na kuja na ubunifu wa kwenda katika maeneo ya wanaomiliki idadi kubwa ya vyombo vya moto, kwa ajili ya kukagua vyombo vyao.

Aidha, alisema ni muhimu wananchi kuendelea kuelimishwa kuhusiana na sheria za usalama barabarani pamoja na kukemea vitendo vya rushwa kwa askari wachache ambao wanaochafua taswira ya Jeshi la Polisi.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuelekeza maadhimisho hayo kitaifa kufanyika Mkoa wa Arusha, huku akitoa wito kwa wadau wa usalama barabarani, kushikamana, kujitoa kwa pamoja ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa hali ya amani na utulivu.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi, Justine Masejo, alisema kama watumiaji wa vyombo vya moto, watafuata kauli mbiu ya utii wa sheria bila shuruti, ni wazi kuwa itapunguza ajali nyingi za barabarani, ambazo zimesababisha watu wengi kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na uharibu wa vyombo vya moto.

Awali, akitoa taarifa fupi kuhusiana na maadhimisho hayo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Mrakibu wa Polisi (SP), Solomon Mwangamilo, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kutoa nafasi kwa Baraza la Usalama Barabarani kufanya tathmini ya jumla kwa mwaka mzima kuhusiana na usalama wa watumiaji wote wa vyombo vya moto.

Alitaja lengo jingine ni kuangalia maeneo ambayo husababisha ajali nyingi za barabarani na kuja na mikakati ya pamoja ya kupunguza ajali hizo.

Kwa mujibu wa Mwangamilo, polisi imetenga maeneo tofauti kwa ajili ya zoezi hilo kwa kuzingatia ukubwa wa Jiji la Arusha.


Alisema zoezi hilo litafanyika katika Vituo vya Polisi, viwanja vya Soweto na kwa wanaomiliki idadi kubwa ya vyombo vya moto watapeleka wakaguzi wa magari kwenda kufanya ukaguzi katika maeneo yao.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad