Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kinondoni, Ramadhani Kingai amesema walichelewa kumkamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa sababu walitaka kujiridhisha uhusika wake katika tuhuma za kupanga kutekeleza ugaidi.
Katika ushahidi wake leo Jumanne Oktoba 26, 2021 Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Kingai ameieleza pia kuwa walichelewa kumkamata Mbowe kwa sababu upelelezi dhidi ya tuhuma zilizomkabili ulikuwa ukiendelea.
“Tulikuwa bado tunaendelea na upelelezi lakini kujiridhisha hasa uhusika wake. Tulikuwa tunafuatilia mawasiliano na uchunguzi wa ki-forensic kuhusiana na tuhuma hizi.
“Taarifa za kuhusika zilikuwa za mwanzo tangu mwezi Julai 2020. Baada ya kukamilisha na kujiridhisha na upelelezi wetu ndipo tulimkamata kuhusiana na tuhuma hizi” amesema Kingai.
“Upelelezi uliokuwa unaendelea dhidi yake ni wa ki-forensic na kupata divices za mawasiliano ili kumuunganisha na makosa haya”
“Kulingana na taarifa kutoka kwa Luteni Urio na vitendo vilivyokuwa vimepangwa, kudhuru viongozi wa Serikali, kufanya vurugu eneo la masoko, kulipua vituo vya mafuta kukata miti kwenye Highway hasa njia ya Iringa ndio maana tulifungua jalada la Makosa ya ugaidi.
Hivi ni vitendo ambavyo vingeweza kuleta taharuki na hofu kwa wananchi kuona hawako salama na vilileta tafsiri ya kosa la kigaidi”