Arusha. Tofauti na siku nyingine alipoletwa mahakamani, juzi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya alionekana mwenye kujiamini na matumaini pale alipoletwa kusikiliza hukumu ya kesi yake kabla haijaahirishwa.
Sabaya, anayekabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha alifikishwa mahakamani saa 3:45 asubuhi kwa kuchelewa, tofauti na siku nyingine.
Kuchelewa huko kulielezwa kumetokana na hitilafu ya gari lililomleta ambalo hata wakati wa kuondoka mahakamani lilikwama tena, hali iliyolazimisha kiongozi huyo wa zamani apandishwa kwenye gari lingine.
Akiwa amevalia fulana nyeupe huku akionyesha uso wa kutabasamu, Sabaya aliwaambia ndugu zake waliofika mahakamani kusikiliza hatima yake kuwa, “watu wa Mungu niombeeni, msiwe na hofu, Mungu atajibu maombi yenu.”
Ukumbi wa Mahakama ulikuwa umefurika watu tofauti na siku nyingine, wakiwamo ndugu wa mshtakiwa huyo, maofisa usalama na makada wa vyama vya siasa.
Mashtaka ya Sabaya, wenzake
Sabaya na wenzake, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, wanakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wanadaiwa kuiba Sh2.769 milioni, mali ya mfanyabiashara Mohamed Saad na Sh390,000 kutoka kwa diwani wa Sombetini, Bakari Msangi katika Mtaa wa Bondeni baada ya kuwatishia kwa bunduki na kuwapiga.
Pia, wanadaiwa kuiba Sh35,000 na simu ya mkononi aina ya Tecno kutoka kwa Ramadhan Rashid.
Endapo watatiwa hatiani, Sabaya na wenzake watakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka isiyopungua 30 jela.
Juzi, mama yake Sabaya alionekana kuwa mwenye huzuni nyingi huku akilia, tofauti na siku nyingine alipohudhuria kesi dhidi ya mwanawe.
Alionekana kububujikwa machozi ndani ya chumba cha Mahakama na nje baada ya kesi kuahirishwa.
Hata hivyo, baada ya kesi kuahirishwa, watu waliendelea kubaki katika viwanja vya Mahakama, huku Sabaya na washtakiwa wengine wakiwapungia mikono ikiwa ni ishara ya kuwaaga wakati wakirudishwa mahabusu.
Ulinzi ulikuwa umeimarishwa nje na ndani ya Mahakama, huku baadhi ya askari magereza wakiwa wamepanda juu ya mapaa ya majengo ya mahakama. Hukumu hiyo ilitarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Odira Amworo baada ya kusikiliza kesi dhidi ya Sabaya na wenzake wawili kwa miezi miwili na nusu.
Hatima ya Sabaya ilikuwa inasubiriwa kwa hamu na watu wengi kutokana na umaarufu aliojipatia wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai kutokana na staili yake ya uongozi iliyowagusa watu wengi kwa namna tofauti.
Tangu kufikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 4, kesi dhidi ya Sabaya imekuwa ikivuta watu wengi wa Arusha na maeneo ya jirani.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Amalia Mushi aliahirisha hukumu hiyo, akisema haiyajakamilika