Samia Auma na Kupuliza Akitoa Vigezo Mji wa Moshi Kuwa Jiji




Hotuba ya Rais, Samia Suluhu Hassan ilikuwa ni ya kung’ata na kupuliza katika masuala makuu matatu, likiwamo la kuufanya mji wa Moshi kuwa jiji, huku akitoa vigezo vya namna mji huo unavyoweza kupatiwa hadhi hiyo.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika jana, Rais Samia alizungumzia pia maombi ya wabunge kuhusu barabara fupi za lami, akisema mkoa huo itabidi usubiri kwanza.



Katika mkutano huo, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Ummy Mwalimu, Mbunge wa Same Magharibi, Dk Mathayo David na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi walionekana kumpigia chapuo Rais Samia kuhusu Urais 2025.



Kabla ya mkutano huo wa hadhara uliohudhuriwa pia na mawaziri watatu, naibu waziri mmoja na wabunge wa mkoa Kilimanjaro, Rais alizindua ujenzi wa barabara ya lami ya Sanyajuu-Elerai na kuweka jiwe la msingi katika daraja la Rau.



Pia, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Kilimanjaro ya Mawenzi na kueleza kuwa mkwamo wa ujenzi huo sasa umeondoka na Serikali itatoa fedha ili ujenzi ukamilike.



Akizungumzia Moshi kuwa jiji, alisema, “... hapa inabidi tuangalie vizuri. Mji wa Moshi unadaiwa kuwa jiji lakini vile vile Vunjo wanataka kuwa halmashauri. Lakini ukitoka Moshi kwenda Vunjo ni kilometa si zaidi ya 20 au 25



“Sasa ama Vunjo ivunjwe tufanye jiji litanuke... Lakini kuna suala pia la vigezo ambalo tukiangalia mji wa Moshi haujafikia. Lakini niwaambie Serikali tutalifanyia kazi,”alisema Rais Samia.



Aliongeza: “Tutaangalia yote kuvunja Vunjo iingie jijini au jinsi tutakavyoona inafaa kulingana na vigezo vilivyopo. Lakini la pili ni la kufufua viwanda. Tukisema Tanzania ya viwanda tunataka viwanda vyote vilivyopo nchini vifanye kazi.”



Kuhusu maombi ya wabunge ya barabara fupi fupi za lami, Rais Samia alianza kwa kuwapa hadithi ya mtu ambaye alipata ajali ndogo kidole kikaumia akawa analia atavaaje pete.



“Lakini alisahau kwamba kuna wanadamu wengine hata kidole cha kuvaa hawana. Sasa ndio haya ya wabunge wenu wa Kilimanjaro. Kila mtu analilia barabara ya lami kilometa saba wakati maeneo mengine ya Tanzania kuna vumbi kilometa 200”



“Moshi mtasubiri kidogo kwa vile barabara zinapitika, zile kilometa sabasaba uchumi ukikua zaidi tutakwenda huko. Lakini kwanza tunatandaza kwa Tanzania nzima kwanza wote angalu tuwe na barabara za changarawe kabla ya lami”



“Sera yetu baada ya kuunganisha mkoa kwa mkoa Tanzania, tulisema tunaunganisha wilaya kwa wilaya. Hiyo kazi bado tunaendelea nayo. Lakini tukasema tunakwenda na barabara za vijijini ili mazao yatoke,” alisema.



Rais alizungumzia pia suala la tozo za miamala akisema kwa kipindi cha miezi mitatu, vituo vya afya karibu 200 vinajengwa na madarasa 500 yamejengwa, na kusema kama nchi ni lazima iwe na chanzo chake cha mapato badala ya kusubiri wahisani.



Pia Rais alizungumzia ombi la Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi aliyetaka wananchi kupewa jukumu la kutunza msitu wa nusu maili, huku akisema ikiwa hilo likiruhusiwa, litaathiri mazingira ya Mlima Kilimanjaro.



“Nataka niwaambie shughuli za wanadamu ni lazima ili tupate maisha lakini na shughuli za kuhifadhi maeneo yetu yana ulazima pia. Eneo lile linahifadhi nzuri tunahifadhi mlima Kilimanjaro,”alisema Rais Samia na kuongeza kusema;-



“Wakati wa Royal Tour tuliuzunguka mlima si chini ya mara tano au sita na kuchukua picha. Hali ya mlima wetu kule sio nzuri. Theluji inayeyuka na mlima wetu unamong’onyoka. Sasa tusipotunza huku chini tukapanda miti ya kutosha”



“Niwaombe wananchi twende kutunza yale maeneo. Tutunze mazingira ili mlima wetu ubaki na hali yake na theluji iweze kurudi ili iwe na sifa ileile inayotuletea wageni wengi,”alisisitiza Rais Samia.



Walichokisema wabunge

Walipopata nafasi ya kuzungumza kabla ya Rais kuongea, wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro waliipongeza Serikali ya awamu ya sita, kwa namna ilivyomwaga fedha za miradi ya maendeleo na kusema hiyo haijawahi kuonekana awamu nyingine.



Hata hivyo, wabunge hao walijikita zaidi katika changamoto ya maji na barabara huku Mbunge wa Moshi mjini, Priscus Tarimo akitaka viwanda ambavyo havifanyi kazi, serikali ivitwae upya.



Mbunge wa Vunjo, Dk Kimei aliomba jimbo la Vunjo liwe na halmashauri yake, huku Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo akiomba mradi wa hospitali ya wilaya, kituo kipya cha mabasi na kukamilika kwa mradi wa maji wa Mwanga-Same.



Akijibu masuala hayo, Rais Samia alisema serikali imechukua changamoto hizo na inakwenda kuzifanyia kazi na pia akaagiza mabango yote ambayo wananchi walikuja nayo, yakusanywe na kwamba atakwenda kuyasoma na kuja na majibu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad