Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema amewataka viongozi mbalimbali serikali kwenda kutumikia wananchi kuleta maendeleo huku akisisitiza kuwa hatarajii kuona mkuu wa mkoa anakuwa mla rushwa na kugeuka Miungu watu.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 11,2021 wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema.
“Uongozi ni dhamana siyo zawadi..tunategemea viongozi mtakuwa mfano, sitegemei kuona mkuu wa mkoa anaingia kwenye vitendo vya rushwa, sitegemei kuona wakuu wa mikoa mnakuwa Miungu watu huko mliko, mpo kule kutumikia watu, siyo watu wawatumikie nyie. Naomba mkafanye kazi tulizowatuma,” amesema Rais Samia.
“Samia Suluhu ninakotoka hakuna makabila, mimi sina kabila, mwalimu Nyerere hakuwa na kabila.. kwenye utendaji wangu wa kazi ukilikoroga nakutumbua bila kuangalia kabila, anayekosea nitamuondoa, sipangi kwa kuangalia kabila, napanga kwa uwezo wake ili kwenda kusaidia wananchi kuleta maendeleo.
Mimi kwenye utendaji wangu wa kazi sina Kabila, uwe Mmakonde uwe mnani ukikosea kwenye kazi Mimi na wewe wala sitokufumbia jicho, sasa kama umetoka ulikotoka ukitumbuliwa ‘Mimi wa Kabila fulani’ hiyo sumu mnaipeleka sana, naomba isimame.”,amesema Rais Samia.