Serikali ya Tanzania yabanwa zuio mikutano ya kisiasa, yajibu




SERIKALI ya Tanzania, imesema haizuii mikutano ya vyama vya siasa bali mikutano inayozuiwa ni ile yenye viashiriavya kuhatarisha usalama wa nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza…(endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili, tarehe 17 Oktoba 2021, jijini Mwanza na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akijibu swali la Mhariri wa Gazeti la Nipashe Kanda ya Ziwa, Richard Makole aliyehoji msimamo wa Serikali dhidi ya zuio la mikutano ya vyama hivyo.

“Kwa mujibu wa katiba yetu vyama vya upinzani vimeruhuswa kisheria, lakini tumeona wakati fulani hata wengine kukamatwa wakati wanafanya mazoezi ya kukimbia. Imekuwa ngumu kukutana kwa namna yoyote ile,”

“Iwe chumbani, kwenye ukumbi, wanakamatwa. Nini msimamo wa Serikali kwamba kukutana ni kosa la jinai au nini kifanyike ili na wao waweze kukutana wafanye mambo yao?” ameuliza Makole.


 
Akijibu swali hilo, Msigwa amesema “hakuna mkutano wa mwanasiasa ulizuiwa, kilichopo ndugu yangu Richard ni utaratibu.”

“Hakuna mkutano wa mwanasiasa uliozuiwa na sio mkutano tu, shughuli yoyote ambayo vyombo vya ulinzi na usalama vitagundua vinahatarisha usalama na vyenyewe vinawajibu kwa mujibu sheria kuzuia shughuli hiyo,” amesema

Msigwa amesema, vyombo vya ulinzi na usalama vina mamlaka ya kisheria kuzuia shughuli yoyote yenye viashiria vya kuhatarisha usalama wa nchi.


“Na sio lazima mkutano, unaweza kwenda kufanya birthday yako lakini hawa ni watalaamu wameshagundua kwamba kwa kufanyika birthday tutahatarisha kitu fulani. sheria inawaruhusu na ndiyo jukumu lao hawawezi wakaacha mkafanya harafu likapigwa bomu mkafa mkasema Polisi walikuwa wapi, wazembe hawakujua, hivyo wanaahukua tahadhari,” amesema Msigwa na kuongeza:

“Na hii sio kwa vyama vya siasa peke yake, vyombo vina malaka ya kusimamia usalama wa nchi wanapogundua kwamba sehemu fulani kuna viashiria vya kuhatarisha usalama vina mamlaka ya kuzuia hatari kutokea, kama walizuia kwenye kukimbia sijui ilikuwaje lakini hayo ni mamlaka ya kisheria ya vyombo vyetu vya kiusalama.”

Mwanzoni mwa Oktoba 2021, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, liliwakamata watu tisa ikiwemo wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kosa la kufanya mazoezi ya kukimbia (Jogging), katika Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe mkoani Dar es Salaam.

Wanachama hao wa Chadema walikamatwa ikiwa ni takribani wiki mbili kupita tangi jeshi hilo la polisi Kinondoni, kuwazuiwa wanawake wa chama hicho (Bawacha), waliotaka kufanya mazoezi na kuziwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad